Habari Mseto

Wakazi wa Kariminu waandamana kushinikiza wapewe ajira katika mradi wa Kariminu 11

November 5th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kariminu, eneo la Gatundu Kaskazini, wanawalaumu wasimamizi wa kampuni ya China ambayo inaendesha mradi wa bwawa la Kariminu 11.

Wakazi hao wanalalama ya kwamba ahadi iliyotolewa na viongozi wao kuwa watapewa kazi hapo imekiukwa.

Tayari serikali imehamisha wakazi wa eneo hilo na kuwapa fidia ili mradi huo uendelee bila tatizo.

Hivi majuzi Waziri wa Maji Bw Simon Chelugui na viongozi wa eneo hilo walizuru mradi huo ili kujionea jinsi inavyeendelea.

Wakati wa ziara hiyo wakazi wa eneo la Gatundu Kaskazini, waliahidiwa hadharani kuwa wao ndio watatangulia kupata ajira katika mradi huo, lakini jinsi mambo yalivyo ni kinyume kabisa.

Watu hasa walioathirika kabisa na ahadi hiyo ni madereva ambao wana ujuzi kamili wa kuendesha magari makubwa; malori.

Bw Karanja Wabuto ambaye ni mkazi wa kijiji cha Gituamba anadai ya kwamba siku cha zilizopita alikwenda katika eneo la mradi huo na kufanyiwa majaribio ya kuendesha lori kubwa la kubeba mchanga.

“Ama kwa hakika nilifuata maagizo yote niliyotakiwa nitimize ya kubeba mchanga eneo moja hadi lingine. Baadaye mhandisi mkuu wa China aliniambia ningoje matokeo kwani walisema wataniita mara moja,” alisema Bw Wabuto.

Hadaa

Anasema hiyo ilikuwa ni hadaa ya hali ya juu kwa sababu baada ya siku chache wahandisi hao waliwaajiri madereva wengine kutoka sehemu zingine ambao sio wakazi wa hapa.

Mkazi mwingine wa Gituamba, Bw John Kariuki anasema wanapitia masaibu mengi kwa sababu walilazimika kubeba hata vyeti vyao vyote pamoja na leseni ya kuendesha gari.

“Sisi kama wakazi wa hapa Gatundu Kaskazini tumechezewa shere kwa sababu hakuna mkazi ambaye anaajiriwa hapa; yote tunayoshuhudia ni wageni kutoka nje ndio wanapewa kazi katika mradi huu muhimu,” alisema Bw Kariuki.

Akaongeza: “Sisi wakazi wa hapa hatuna fujo yoyote na kile tunaomba zaidi ni kuona ya kwamba haki imetendeka kwetu kama watu wa hapa. Tunachokamia sana ni kupata ajira.”

Wakazi hao wanaitaka serikali na viongozi wa eneo hilo waingilie kati ili kuona ya kwamba wanapata ajira haraka iwezekanavyo.