Habari Mseto

Wakazi wa Kiandutu wadhihirisha 'tukipata mikopo tunaweza'

April 25th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Kiandutu na vitongoji vyake wamehimizwa kujiunga pamoja ili waweze kupokea mikopo ya Uwezo Fund.

Mbunge wa Thika, Mhandisi  Patrick Wainaina aliyezuru eneo hilo mnamo Jumanne ili kujionea mwenyewe miradi kadha inazoendeshwa na  vikundi kadha kwa lengo la kujiendeleza kimaisha.

“Mimi lengo langu sio kupatia mtu binafsi pesa. Kile ninataka kuona ni mkijiweka kwa vikundi ili kuanzisha miradi tofauti. Iwapo mtafanya hivyo, niko tayari kutoa fedha za kujiendeleza kibiashara za Uwezo Fund,” alisema Bw Wainaina.

Alisema lengo lake kuu lilikuwa kujionea miradi tofauti za maendeleo zinazoendeshwa na  wakazi hao wa Kiandutu baadaye alikuwa tayari  kuwapa fedha zaidi ya  kuendelea na miradi hizo.

“Ninafuraha kuona ya kwamba wakazi wa Kiandutu wamejitolea kuanzisha miradi tofauti itakayowainua kimaisha,” alisema Bw Wainaina.

Alisema maendeleo hupatikana tu iwapo watu watajikusanya pamoja na kuamua ni jambo lipi zuri wataendesha na litakalowafaidi kimaisha.

Eneo la kwanza kuzuru ili kujionea jinsi watu wanajikimu kimaisha lilikuwa ni katika kikundi cha Exodus cha kuunda vifaa vya mbao.

Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye ni seremala kwa miaka 20 Bw Benson Kamande Njuguna, anasema ameweza kukuza kikundi cha vijana 18 ambao sasa wengi wao wanaunda masofa, viti, vitanda na hata kabati.

“Sisi kama kikundi hiki cha Exodus tunajivunia kujiendeleza ambapo hata vijana wengi wameweza kuunda vifaa vya mbao vinavyotamanika na wengi. Nimeweza pia kuwanoa vijana wengi ambao wengi wao walikuwa wahuni lakini sasa ni raia wema,” alisema Bw Njuguna.

Bw Peter Muturi ambaye ni mwanachama wa kikundi hicho anasema hapo awali alikuwa mhuni ambaye alipora mali ya watu jijini Nairobi, lakini sasa yeye ni mzalendo aliyegeuka na kuwa mpole na mnyenyekevu.

“Tangu niache mambo maovu katika jiji la Nairobi, niliamua kuingilia kazi ya useremala na ndiyo sasa inanilisha. Sitegemei vya bure tena,” alisema Bw Muturi.

Kikundi kingine kilichojitolea ni kile cha wanawake wasioona ambao ni vipofu lakini wanaendesha miradi ya ususi na ufugaji wa mbuzi.

Kwa sasa wamefuga mbuzi wapatao kumi.

Huku wakiwa wameajiri watu wa kuwafanyia kazi hizo wameonyesha wazi kuwa wanaweza kufanya kazi yoyote inayoendeshwa na watu wasio walemavu.

Kikundi kingine cha wanawake kiko katika eneo la Kimathi ambapo wanafuga mbuzi kumi na wana matumaini ya kuongeza zaidi.