Habari Mseto

Wakazi wa Korogocho wanufaika na mitungi ya maji na vieuzi

April 4th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Bidco Africa Ltd na Shirika la Ghetto Classic zimeshirikiana kugawa mitungi ya maji na dawa ya vieuzi kwa wakazi wa mtaa wa Korogocho, jijini Nairobi.

Mwakilishi wa kampuni ya Bidco Africa Ltd Bw Willys Ojwang’, alisema kampuni hiyo ilijitolea kwa dhati kuona wakazi Wa Korogocho na vitongoji vyake, wakinufaika.

“Tunajaribu kufikia wakazi wapata 300,000, lengo letu kuu ni kudumisha usafi ili kupambana na homa corona,” alisema Bw Ojwang’

Alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanafikia wakazi wengi katika vijiji vingine tisa jijini Nairobi.

“Janga hili la corona limekuwa tisho kubwa ulimwengu mzima na kwa hivyo ni vyema kuwahamasisha wananchi,” alisema Bw Ojwang’.

Aliwahimiza wakazi hao wadumishe usafi kwa kunawa mikono kila Mara ili kupambana na janga hilo.

Alitoa mwito kwa wahisani wengine popote walipo wajitolee ili kuwajali wakazi wa vitongoji duni hasa jijini Nairobi.

Tayari kampuni ya Bidco Africa imefanya ushirikiano na kampuni ya maji ya Thiwasco water Company kwa kutoka vieuzi na Mitungi ya maji 100, huku wenzao wakisambaza maji kwa wingi mjini Thika na vitongoji vyake.

Wakazi wa Korogocho wakihamasishwa jinsi ya kunawa mikono. Picha/ Lawrence Ongaro

Wahisani wengine ambao wamefanya juhudi ya kusaidia wananchi ni Vishal Oshwal, Mama Millers, Broadway na Equity Bank tawi la Thika.

Baadhi ya wale waliinufaika na ufadhili huo ni sekta ya Matatu, wanabodaboda, hospitali, na kituo cha polisi cha Thika.

Alisema wataendelea kuzuru maeneo mengine ili kusambaza vieuzi ( sanitizer) kwa wananchi.

Alisema kwa wiki tatu sasa wananchi wamefuata mwito wa kunawa mikono jambo ambalo alisema litasaidia kupambana na Corona.

“Tunajua vyema homa ya Corona ni hatari kwa binadamu na kwa hivyo ni jukumu la kila mmoja kukabiliana nalo,” alisema Ojwang’.

Alitoa mwito kwa wahisani wengine popote walipo kujitokeza ili kusaidia kwa chochote walicho nacho ili kukabiliana na janga hilo.