Habari Mseto

Wakazi wa Lamu watakiwa kupanda miti maeneo wanakoishi

April 2nd, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

SHIRIKA la Uhifadhi wa Misitu (KFS) katika Kaunti ya Lamu limehimiza wakazi kujihusisha na upanzi wa miti kwenye maeneo wanayoishi.

Afisa Msimamizi wa KFS eneo la Lamu, John Mbori, anasema hatua hiyo itasaidia pakubwa kupunguza visa vya uharibifu wa misitu na mazingira kwa jumla hata baada ya kuondolewa kwa marufuku iliyopo dhidi ya ukataji  miti kote nchini.

Afisa wa KFS wa kaunti ya Lamu, John Mbori. Amewataka wananchi kupanda miti kwenye makazi yao ili kukabiliana na uharibifu wa misitu ya serikali. Picha/ Kazungu Kalume

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Mbori alisema ranchi na misitu mingi ya serikali na hata ile ya kijamii imekuwa ikiharibiwa na wakataji miti eneo la Lamu kutokana na kwamba wakazi hao hawana miti kwenye sehemu zao wanazoishi.

Alisema ikiwa kila mkazi atajitahidi kupanda na kumiliki miti yake mwenyewe, basi azma ya serikali ya kupiga marufuku ukataji miti kote nchini itafaulu hata zaidi.

Magunia ya makaa yaliyonaswa na kupelekwa katika kituo cha KFS mjini Witu. Picha/ Kalume Kazungu

“Ukataji miti ambao umekuwa ukiendelezwa kwenye misitu ya serikali na ile ya kijamii pamoja na ranchi mbalimbali hapa nchini unatokana na sababu kwamba watu hawana miti kwenye makazi yao.

Ningewahimiza wakazi kupanda miti yao wenyewe majumbani. Wakifanya hivyo itakuwa rahisi kwao kufikia asasi husika za serikali na kuomba kibali ili waweze kukata miti yao na kuuza. Ikiwa hili litaafikiwa, ninaamini ukataji miti kiholela kwenye misitu yetu ya serikali utapungua au hata kusitishwa kabisa,” akasema Bw Mbori.

Wachomaji makaa wakipakia magunia ya makaa kwenye lori la polisi baada ya kukamatwa msituni Boni. Picha/ Kalume Kazungu

Kauli ya afisa huyo inajiri siku chache baada ya idara ya usalama ya Lamu kunasa magunia zaidi ya 240 ya makaa na shehena za mbao ndani ya msitu wa Boni.

Majuma mawili yaliyopita, maafisa wa usalama pia walinasa mbao za mti aina ya Bambaru ambazo thamani yake ilikadiriwa kuwa Sh 800,000.

Mbao hizo zilinaswa eneo la Maisha Masha, tarafa ya Witu, Kaunti ya Lamu.

Mapema juma lililopita, idara ya usalama ya kaunti ya Lamu, ikiongozwa na Kamanda Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Muchangi kioi, ilizindua operesheni maalum inayolenga kuwasaka wachomaji makaa na wapasuaji mbao ndani ya msitu wa Boni.