Wakazi wa Likoni Flats walalama kuhusu uhamisho

Wakazi wa Likoni Flats walalama kuhusu uhamisho

NA FARHIYA HUSSEIN

WAKAZI katika nyumba za kaunti zilizo mtaa wa Likoni Flats, Kaunti ya Mombasa, wameibua malalamishi kuhusu makataa waliyopewa na Serikali ya Kaunti kuhama ili nyumba zao zifanyiwe ukarabati.

Serikali ya Kaunti ilikuwa imewapa muda hadi Juni kuhama ili ukarabati wa nyumba hizo ufanywe chini ya mpango maalumu unaolenga kukarabati mitaa takriban 11 ya Mombasa.

Taifa Leo imebaini kuwa mradi huo unaotarajiwa kuanza katikati ya mwaka huu, utawaathiri zaidi ya wakazi 300 ambao wanatakiwa wawe wamehama kufikia Juni.

Katika mahojiano na Taifa Leo, walisema wanataka fidia isiyopungua Sh250,000 kwa kila mpangaji.

Mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Bi Teckla Mjomba, alisema pesa zinazopendekezwa kuwa walipwe hazitatosha kuhamia kwingine kwa vile kodi za nyumba katika mitaa mingine ni ghali kwa wakazi hao.

“Tuliona kile kilichotokea kwa wenzetu katika mradi wa kujenga nyumba mpya mtaa wa Buxton. Nimesikitishwa sana, tulikutana na Gavana mwezi Desemba pale Wild Waters tukaeleza kero zetu lakini bado tunasubiri majibu,” akasema.

Mpangaji mwingine, Bi Joyce Lewa alisema mazungumzo kati yao na serikali ya kaunti yamekuwa yakiendelea kwa miaka sita.

“Tunaitaka kaunti itupe muda kujipanga. Baadhi yetu tuna watoto ambao wako shuleni na tunahitaji kujipanga kwa uhamisho wao. Pia, tunaomba kuongezwa kwa ada ya fidia kwa sababu mimi binafsi nimekarabati nyumba ninayoishi,” akasema Bi Lewa.

Serikali ya kaunti ilithibitisha kuwa ilipanga kuwalipa wakazi hao fidia kulingana na kiwango cha kodi wanacholipa kila mwezi.

Afisa Mkuu wa Ardhi katika kaunti, Dkt June Mwajuma, alisema kiasi cha fidia kitakuwa ni mara mbili ya kiasi wanacholipa kama kodi kwa miaka miwili.

Wakazi hao hukodisha nyumba hizo kwa kati ya Sh2,800 na Sh4,400 kila mwezi, kulingana na ukubwa wa nyumba.

Kulingana na afisa huyo, mazungumzo na wakazi hao kuhusu malipo ya fidia bado yanaendelea.

“Baada ya makubaliano na wakazi hao ujenzi utaanza mara moja,” alisema Dkt Mwajuma.

Aliongeza kuwa ukarabati utakapokamilika nyumba zitauzwa huku kipaumbele kipeanwa kwa wapangaji wa eneo hilo.

“Mradi huu unatekelezwa kupitia kwa mkataba wa maelewano kati ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa na mjenzi ambaye ni kampuni ya Goldland Incorporated Limited. Mradi utagharimu Sh8 bilioni. Takriban nyumba 3,200 zitajengwa,” akasema.

Serikali ya Kaunti inaendeleza mipango ya ujenzi upya na ukarabati wa nyumba kuukuu katika mitaa takriban 11 ya Mombasa.

Mitaa ambapo nyumba zilishabomolewa kufikia sasa ni Buxton na Mzizima.

  • Tags

You can share this post!

Base Titanium yaongeza juhudi za kutunza ardhi

Majaji kupewa ulinzi zaidi baada ya shambulio

T L