Habari Mseto

Wakazi wa Magumoni Kiambu kuhamishwa kupisha ujenzi wa soko

August 29th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA 70 katika kijiji cha Magumoni katika Kaunti ya Kiambu watalazimika kuhama kutoka makazi yao ya sasa ili soko la kisasa lijengwe.

Waziri wa Viwanda wa Kaunti ya Kiambu Bw Kigo Njenga alisema tayari kaunti imetoa ilani ya kuwajulisha wakazi hao wahame mara moja.

Hata hivyo wakazi hao walipinga hatua hiyo wakisema walinunua mahali hapo miaka za 90 na tayari wana vyeti vya kuumiliki ardhi hiyo.

Bw Njenga alisema ujenzi huo umedhaminiwa na serikali kuu kwa ushirikiano na Kaunti ya Kiambu.

“Eneo hilo ni mali ya umma na kwa hivyo huko ndiko imependekezwa kujengewa soko hilo la kisasa,” alisema Bw Njenga.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi katika kijiji cha Magumoni alipozuru eneo hilo kusikiza maoni ya wakazi hao.

Hata hivyo wafanyabiashara wengi na wakazi waliohudhuria mkutano huo walipinga hatua hiyo ya serikali ya kuwafurusha wakisema ni ya kinyama kwa sababu wamekuwa mahali hapo kwa zaidi ya miaka 20.

Mfanyabiashara David Mungai alipendekeza soko hilo lijengwe nyumba ya maduka ya sehemu hiyo ili kuzuia hatua ya kuwafurusha.

“Tunaiomba serikali isitishe hatua ya kuwafurusha wakazi wa hapa na itafute pahala pengine hata kama ni karibu na barabara kuu,” alisema Bw Mungai.

Mkazi mmoja katika kijiji hicho aliisihi serikali iwaache waendelee na maisha ya kawaida badala ya kuwahangaisha bure.

“Wengi wetu hapa hatuna kazi za kudumu isipokuwa hizi za kibarua, na kwa hivyo hatuna pahala pengine pa kwenda iwapo tutafurushwa,” alisema Bw Joram Chege ambaye ni mkazi wa huko.

Mwakilishi wa jamii ya Wakikuyu Bw Thiong’o wa Gitau aliwashauri wakazi hao kufuata maagizo ya serikali kwa sababu soko hilo litasaidia kizazi kijacho katika siku za usoni.

“Huu ni mradi wa maendeleo endelevu na kwa hivyo ni sharti wananchi wafuate maagizo ya serikali. Hata ninatarajia kuhama hivi karibuni ili nitafute pahala pengine pa kwenda,” alisema Bw Gitau ambaye ni chifu aliyestaafu.