Habari Mseto

Wakazi wa Matungu waamua kuua washukiwa wa mauaji

May 12th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

WAKAZI wa eneobunge la Matungu wameamua kuwachukulia hatua wahalifu ambao wamekuwa wakiwahangaisha kwa muda mrefu.

Wahudumu wa bodaboda Ijumaa waliua washukiwa wawili wa mauaji ambayo yameshuhudiwa katika eneo hilo kwa karibu mwezi mmoja sasa.

Hayo yalitokea huku polisi wakidai wahudumu wa bodaboda huhusika katika uhalifu huo ambao umetia hofu wengi katika Kaunti ya Kakamega.

Kwa jumla, washukiwa wanne wa uhalifu wameuliwa kwa kipindi cha wiki moja.

Kwenye kisa cha Ijumaa, Bw Wycliffe Mukabana kutoka eneo la Ekero, Mumias Mashariki na Bw James Mukhwana kutoka Namulungu, Matungu walishambuliwa na wahudumu wa bodaboda wenye ghadhabu ambao waliwapiga kwa mawe na rungu.

Mukabana aliuawa katika eneo la Emuberi huku Mukhwana akipigwa mawe hadi kufa katika eneo la Namulungu. Ijumaa iliyopita, washukiwa wawili waliuawa katika vijiji vya Mayoni na Ejinja.

Afisa Mkuu wa Polisi wa Matungu, Bw John Matsili alisema miili ya waliouawa ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Bungoma.

“Ninakemea vikali mauaji hayo ya kinyama. Inasikitisha kwamba wananchi wameamua kuua washukiwa. Wasipozuiliwa, wataishia kuua raia wasiokuwa na hatia,” akasema.

Kwa mwezi mmoja sasa, wakazi wa Matungu wamekuwa wakiishi kwa hofu kwani kuna genge la majambazi ambalo limeshambulia na kuua watu wasiopungua 13 wakiwemo watoto watatu.

Kuna wakazi wengine wengi ambao wanauguza majeraha baada ya kushambuliwa na genge hilo.

Polisi walimkamata mwanamume anayeaminika kuwa kiongozi wa genge husika na wanaamini atawasaidia kwenye juhudi zao za kukomesha uhalifu unaoendelea.

Kamishna wa Kaunti ya Kakamega, Bw Abdulrizak Jaldesa alisema polisi wanadhibiti hali na hivi karibuni, wakazi wa Matungu wataendelea kuishi bila hofu.