Habari

Wakazi wa Mayungu waliotegemea dampo kupata chakula wapokea msaada kutoka kwa madaktari

June 10th, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

SIKU chache baada ya Taifa Leo kuchapisha makala kuhusu mahangaiko ya baadhi ya wakazi wa Mayungu, Kaunti ya Kilifi, madaktari wamejitokeza na kuwasaidia wakazi hao.

Chapisho hilo lilieza kuwa wakazi wa eneo hilo hutegemea dampo kupata chakula.

Taifa Leo ilipata fursa ya kumhoji Dkt Salma Naji kutoka Malindi ambaye ni miongoni mwa wale waliotoa msaada kwa wakazi hao.

“Tulizuru eneo hilo na katika kujaribu kupambana na janga la Covid-19, mimi na timu yangu tukaandamana na wataalam kutoka Malindi kutoa msaada wa ndoo, mitungi na sabuni kwa wakazi wa kijiji cha Mayungu,”akasema Dkt Naji.

Wakazi wa Mayungu waliotegemea dampo kupata chakula wapokea msaada kutoka kwa madaktari. Picha/ Farhiya Hussein

Pia anasema waliandaa hamasisho kuhusu afya, lakini watoto waliwasimulia machungu wanayopitia kiasi cha kuibua hisia za huzuni.

“Mvulana wa takriban umri wa miaka 10 alisimama na majibu yake mwanzoni yalinitia tabasamu usoni mwangu lakini kilichosikitisha ni simulizi yake kuhusu jinsi ni kawaida kwao kila waamkapo kusubiri lori la chakula. Sote tulidhani kwamba kuna mtu huja kila siku kusambaza chakula kwenye lori. Walakini tuligundua lori linaloitwa la chakula ni lori la taka,” akasikitika Dkt Naji.

Dampo hilo ni eneo ambalo taka zote kutoka mji wa Malindi hutupwa.

Familia hizi pamoja na akina mama wajawazito, wazee na watoto hutegemea kile kinachotupwa hapo kama chakula na hata chanzo cha mapato.

“Siku iliyofuata kazini tulizungumza na wenzetu na kupata pesa za kutosha kununua mikate 200 ambapo tulirudi Mayungu kutoa mgao,” alielezea Dkt Naji.

Anasema walifika muda mwafaka kushuhudia hali hiyo ya kusikitisha.

“Tulifika kwa wakati mwafaka kuona lori la taka likiwa pahala hapo. Wanakijiji walianza kutoka ndani ya nyumba zao wakiwa na ‘fimbo’ ndefu za vyuma ambazo walitumia kuchakura taka na kutafuta chakula, chupa za plastiki na glasi,” akasimulia.

Anasema Dkt Naji, kuwa wakazi hao wanauza chupa hizo kupata pesa kidogo ambapo chupa za plastiki huuzwa Sh5, za glasi kwa Sh10 hadi Sh15 .

Wakazi wa Mayungu waliotegemea dampo kupata chakula wapokea msaada kutoka kwa madaktari. Picha/ Farhiya Hussein

“Niliporudi nyumbani nilichukua hatua ya kuzungumza na marafiki kadhaa ikiwemo Bi Jimia Abdul kutoka Mombasa na Dkt Omar Tayari kutoka Amerika. Tulianzisha akaunti ya kuekeza mchango na ndani ya wiki mbili tulifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh400,000 za Kenya,” anasema Dkt Naji.

Lakini anaeleza kwamba kabla ya kuangaziwa kwa madhila ya watu wa Mayungu, mnamo Mei, 31, 2020, kutokana na msaada wa wanafamilia na marafiki, walifanikiwa kugawa chakula cha thamani ya Sh5,000 kwa kila familia katika maeneo kadhaa kaunti ya Kilifi ambapo walifaa familia 100.

“Bado kuna familia zingine 80 hadi 100 ambazo bado zinahitaji msaada. Kwa kushirikiana na wanakijiji tunatumai kuanzisha njia bora ya kudumu. Ni tumaini letu na maombi kwamba tunapata watu wengi wenye busara iwezekanavyo kusaidia familia hizi,” akasema Dkt Naji.