Habari za Kitaifa

Wakazi wa Mradi, Embakasi walivyokurupuka tena Jumatatu kwa hofu ya mlipuko mwingine

February 5th, 2024 1 min read

NA WAANDISHI WETU

KIZAAZAA kilizuka asubuhi ya Jumatatu, Februari 5, 2024 katika kijiji cha Mradi, Embakasi ambacho kilikumbwa na mkasa wa mlipuko wa gesi Ijumaa, kufuatia kile kilichodaiwa kuwa kuvuja kwingine kwa gesi.

Wakazi katika eneo hili waliripoti asubuhi kwamba walihisi gesi ikinuka kama ile waliyoihisi kwenye pua zao muda mfupi kabla mlipuko mkubwa uliotokea Ijumaa na kuacha watu sita wamefariki na zaidi ya 300 wakipata majeraha mabaya.

Kutokana na hilo, wakazi walianza mikikimikiki, huku familia zingine zikiondoka kwenye makazi yao na kutoroka kufuatia hofu mpya iliyotanda Jumatatu kuhusu uwezekano wa mlipuko mwingine.

Afisa Mkuu wa Kitengo cha kukabiliana na Majanga katika Kaunti ya Nairobi Bwamwel Simiyu aliambia Taifa Leo kwamba eneo hilo limedhibitiwa na kikosi cha zimamoto kilikuwa kimeshatumwa kupambana na hali yoyote ya dharura.

Baadaye, jengo la KQ Pride Center nalo liliagiza wafanyakazi na wahudumu kuondoka kufuatia mkisio wa kuvuja kwa gesi eneo hilo hilo la Mradi, Embakasi.

Usimamizi wa Kenya Airways ulisema ulichukua tahadhari hiyo kwa kuwa jengo hilo limo karibu na eneo la mkasa wa mlipuko wa gesi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi eneo la Nairobi Adamson Bungei aliwatuliza wakazi alipofika eneo hilo, akiwataka kutokuwa na hofu akiwahakikishia kwamba uchunguzi umefanywa na kwamba hakuna matanki mengine yaliyokuwa yanavuja gesi.