Habari

Wakazi wa mtaa wa Karagita walalama 'nguvu za giza' zimezidi

May 25th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa mtaa wa Karagita ulioko katika Kaunti ya Nakuru wameteta kuwa serikali yao ya kaunti inatoa leseni kisirisiri kwa wachawi.

Walisema Ijumaa kuwa serikali ya Gavana Lee Kinyanjui imekuwa ikiwatoza ushuru wachawi na ndio sababu mtaa huo umejaa “nguvu za giza”.

Wakiongozwa na mzee wa kijiji James Otieno, waliambia Taifa Leo kuwa katika kipindi cha miaka miwili sasa, eneo hilo lililoko katika viunga vya mji wa Naivasha limepoteza takriban watu 30 kufuatia athari za uchawi.

Alisema kuwa athari zingine za uchawi ni ndoa kusambaratika, mimba kutoka, wanaume wengine kuishiwa na nguvu za kiume ghafla, ukosefu wa watoto katika ndoa, magonjwa hasi na yasiyotambulika kwenye vipimo vya hospitalini huku wengine wakinyongwa bila kuwaona wavamizi.

“Ni katika msingi huo ambapo tumezindua msako dhidi ya wachawi ambao wanaishi miongoni mwetu. Tumefanikiwa kunasa watatu ambao tumewakabidhi kwa maafisa wa usalama na hatukomi kuwasakama,” akasema Bw Otieno.

Aliongeza kuwa washukiwa hao walikuwa na stakabadhi za usajili wa kaunti kama wafanyabiashara wa kuuza dawa za kienyeji.

Ingawa gavana Lee Kinyanjui amekanusha madai kuwa serikali yake inatambua ushirikina kama suala halali la kijamii, wenyeji wa Karagita walishikilia kuwa wamekuwa wakipokezwa fununu kuwa ukiwa mchawi anayesaka kutambuliwa na serikali hiyo, huwa unasajiliwa kwa ushuru wa Sh5,000 kwa mwaka.

Afisa msimamizi wa utawala eneo hilo Kpl Moses Koech aliambia Taifa Leo kuwa wengi wa mtaa huo huamini ushirikina.

“Baada ya kupokezwa tetesi hizo na wenyeji, nimefanya uchunguzi wangu. Nimebaini kuwa kwa miaka mingi eneo hili limekuwa likiamini uchawi. Wenyeji wamekuwa wakidai kuwa kuna mabasi ya mashamba ya maua eneo hili ambayo yameonekana yakila nyasi usiku. Ni suala la kasumba akilini,” akasema.

Hata hivyo, alikiri kuwa kuna washirikina katika mitaa mingi ya eneo hilo.

“Ndio tuko nao. Na kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi kutekeleza ushirikina, kwa mwaka mmoja serikali imeshtaki washukiwa 14 na ambapo 10 wameachiliwa kwa ukosefu wa ushahidi lakini hao wengine wakifungwa vifungo vya kati ya miezi sita na 14,” akasema.

Alionya wenyeji dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao, akifichua kuwa maafisa wa kiusalama wamekuwa wakinusuru washukiwa kabla ya kuuawa na wenyeji.

Kasisi Godfrey Mbugua wa kanisa la Deliverance eneo hilo alisema kuwa amekuwa akishirikisha uhamasisho wa krusedi na mikesha ili kuwapa wenyeji imani ya Mungu badala ya kuamini nguvu za gizani.

“Niko na maumivu ya kiroho na kusononeka kwingi kuona jamii ikishikilia imani ya nguvu za uchawi. Ni kasumba akilini lakini tunafanya bidii kupambana na uvutio huo. Tunalenga kusajili wengi katika imani ya kweli ya kumtegemea Mungu aliyetupa roho mtakatifu atuongoze kwa nuru. Na tutashinda,” akasema.

Wakenya

Shirika la The Pew Research Center kutoka Marekani mwaka wa 2017 lilitoa ripoti ikionyesha kuwa Wakenya wengi huabudu miungu, hutoa kafara, hushiriki ushirikina na pia kuamini maroho ya kuzimu.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya imo mbele ya mataifa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Nigeria, Zambia na Rwanda katika kuamini ushirikina.

Robo ya Wakenya waliohojiwa wakiwa ni wafuasi wa dini mbalimbali walikubali kuwa huvaa hirizi na pia hutembelea ‘wataalamu’ wa kienyeji ambao wanasifika kwa kupeana juju.

Bw George Ongere ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Center for Inquiry-Kenya anasema wameandaa mikakati ya kuandaa warsha kote nchini kupambana na mitazamo hiyo ya ushirikina.

“Tumepanga mikakati ya kuelimisha Wakenya kuhusu adhari za kushikilia misimamo ya ushirikina,” akasema.

Alisema kuwa mikakati hiyo imeanzishwa katika Chuo Kikuu cha Moi ambapo kikundi kiitwacho Moi Freethinkers kitashirikisha juhudi za kuhamasisha wananchi dhidi ya kuamini mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.

“Hatua kama hiyo inashirikishwa na kikundi kingine kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Kuwatumia wanafunzi wa vyuo vikuu kuna maana kuwa tutapata waelimishaji ambao wana umakinifu wa mawazo ya kisasa,” akasema Bw Ongere.

Aidha, Ongere alisema kuwa wameanzisha jarida liitwalo Skeptical Inquirer, ambalo ni la kupeanwa bure kwa raia ili wajisomee mijadala ya ama kuunga au kupinga mila zinazoambatana na ushirikina.