Habari Mseto

Wakazi wa Muguga Thika Magharibi wataka usalama uimarishwe

March 13th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Muguga eneo la Thika Magharibi, wanalalamika kuhusu uhalifu wa mali ambao unazidi kuendelezwa eneo hilo.

Wakazi hao wanasema kuwa wahalifu hao ambao wanavamia kwa vikundi wamezidi kwa zaidi ya mwezi mmoja mfululizo.

Wakazi wawili ambao ni majirani, Denis Onyango, na John Mwangi, wanasema ya kwamba mnamo Alhamisi usiku wahalifu walivamia maboma yao na kuiba mali ya thamani kubwa.

“Mimi kwangu walifika mwendo wa saa saba za usiku na kitu cha kwanza walichokifanya ni kuzima umeme katika boma langu. Baadaye walivunja mlango wa nyuma wa jikoni na kuiba mtungi wa gesi, masufuria na vyombo vingine muhimu,” alisema Bw Onyango.

Naye jirani John Mwangi, ambaye amefuga kuku alisema kuku wapatao 12 waliibwa na wakaharibu shamba lake lililo nje ya nyumba yake.

Walisema kwa muda wa wiki mbili hivi zilizopita kumekuwa kukinyesha mvua kubwa usiku na kwa hivyo walivamia nyumba zao wakati huo huwa na giza totoro.

Wanazidi kueleza ya kwamba licha ya barabara za eneo hilo kuwa mbovu hata walinda usalama wakielezwa hawafiki haraka.

Wanaomba mkuu wa Polisi eneo hilo achukue jukumu la kuwasaka wahalifu hao ambao wamezidi kuhangaisha wakaaji wa Muguga bila huruma.

Wakazi hao wanazidi keleza ya kwamba tayari wamewasilisha malalamiko hayo kwa mbunge wao ambaye wanaamini atachuka jukumu kuona ya kwamba maisha yao hayako hatarini.

“Sisi kama wakazi wa hapa tumeishi kwa amani kwa muda mrefu lakini ni hivi majuzi tumeanza kuona mambo yakibadilika huku tukikosa usalama wetu,” alisema Bw Peter Macharia ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Walizidi kulalamika ya kwamba wahalifu hao huwa wanajihami na silaha butu kama mapanga, shoka, na vyuma vizito ambapo hata wakivamia boma lako hauwezi kufanya matata.

“Sisi kwa sasa tuko katika hali ngumu kwa sababu hata tunahofia maisha yetu. Hata wengine wetu wanakesha bila kulala ili kungoja wahalifu hao,” alisema Bw Macharia.

Kamanda wa Polisi, kaunti ndogo ya Thika Bi Beatrice Kiraguri, amesema ya kwamba tayari afisi yake imeanzisha uchunguzi mara moja kuhusu malalamiko hayo.

“Maafisa wangu wameanza kupiga doria huku uchunguzi kamili ukiendelea kuhusu malalamiko hayo,” alisema afisa huyo.