Wakazi wa Munyu na Komo kujengewa daraja jipya

Wakazi wa Munyu na Komo kujengewa daraja jipya

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kujenga daraja la kuunganisha vijiji vya Munyu na Komo.

Kwa muda wa miezi mitano sasa watu wanane wamesombwa na maji wakijaribu kuvuka Mto Ndarugo.

Ni baada ya mikasa hiyo ambapo Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro, amesema kuwa chini ya wiki moja daraja litajengwa ili wakazi wa Munyu waweze kuvuka kwa urahisi kutoka upande mmoja hadi mwingine.

“Baada ya kupata habari kwamba watu kadha wamesombwa na maji katika eneo hili, nimefanya juhudi kujionea kinachoendelea hapa na ni lazima daraja la kudumu lijengwe hapa,” alisema Dkt Nyoro.

Kulingana naye, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zitashirikiana pamoja kuona ya kwamba katika kipindi cha chini ya wiki moja daraja la kisasa linajengwa eneo hilo.

Mnamo Jumatatu jioni mwili wa mtu ulipatikana ukielea katika mto Ndarugo ambapo timu kutoka zimamoto katika Kaunti ya Kiambu ilifanikiwa kuuondoa mwili huo.

Akizungumza na wakazi wa Munyu mnamo Jumanne, Dkt Nyoro alisema barabara ya umbali wa kilomita saba ya Muguga- Ngatia-Munyu itakarabatiwa haraka iwezekanavyo ili wakazi wa eneo hili waweze kuendesha biashara zao kwa njia rahisi.

“Ninaelewa kuwa kunaponyesha hali huwa mbaya hasa kwa wafanyabiashara na wahudumu wa matatu na waendeshaji wa bodaboda. Kwa hivyo kazi hiyo itaendeshwa haraka iwezekanavyo,” aliahidi Dkt Nyoro.

Pia aliahidi ataimarisha hospitali ya Munyu ili kufikia kiwango cha Levei 3.

“Ninajua idadi ya wakazi wa Munyu na maeneo ya karibu ni wengi na kwa hivyo ni vyema kupanua huduma ya matibabu ili kutosheleza mahitaji yao,” alifafanua gavana huyo.

Aliahidi kurekebisha soko kuu la Munyu ambalo alisema liko katika hali mbaya.

“Hivi karibuni kazi ya kurekebisha soko hilo itaanza mara moja. Ninaelewa kuna shida ya msongamano na ni vyema kujenga soko la kisasa,” alisema Dkt Nyoro.

You can share this post!

Wanaharakati waweka wazi kile serikali inafaa kufanya kabla...

MAPISHI: Mahamri

adminleo