Habari Mseto

Wakazi wa Murang'a wadai chui yuko maeneo hayo akiwashambulia mbuzi

February 22nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa vijiji vitatu katika eneo la Kigumo, Kaunti ya Murang’a, wanaishi kwa hofu kutokana na chui anayeonekana katika makazi yao.

Vijiji vinavyohofia kuvamiwa na myama huyo ni Kiriti, Gatuya-ini, na Mutunguru.

Wakazi hao waliteta ya kwamba kuna Chui ambaye tayari amewaua mbuzi kadha wakati wa usiku.

“Mnamo Jumatano usiku niliwapoteza mbuzi wangu watatu niliyoletewa na wakwe zangu wiki chache zilizopita. Jambo hilo limesababisha wakazi wengi kuweka mbuzi wao ndani ya nyumba zao ili kuepuka mnyama huyo wa pori kuwaua mbuzi wao,” alisema Bi Hellen Waithera ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kiriti.

Naye Bi Esther Wairimu, mkazi wa kijiji cha Mutunguru alisema ya kwamba mnamo Jumatatu usiku alisikia mbuzi wake wawili wakipiga kelele kwenye zizi na alipotazama kutoka dirishani aliona mbuzi wamelala sakafuni baada ya kuuawa na chui huyo hatari kwa usalama.

“Baada ya kisa hicho kutendeka, wakazi wa hapa wamewasiliana na shirika la KWS ili kuchukua hatua ya haraka. Hata hivyo, shirika hilo linafanya kazi kwa mwendo wa kobe – jambo linalokera wakazi hao. Walisema ya kwamba hata kwa wakati huu wanahofia maisha ya wana wao ambao hurauka alfajiri wakienda shuleni. Tuna wasiwasi kwa sababu watoto wetu hupitia  vichakani wakielekea shuleni. Iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa bila shaka tutalazimika kuwaondoa watoto wetu shuleni,” alisema Bi Wairimu.

Bw Joseph Irungu mkazi wa Mutunguru anasema hivi majuzi akielekea kuchuna kahawa mwendo wa alfajiri alimuona chui huyo kwa hatua ya mbali na jambo la haraka alilofanya ni kurejea nyuma alikotoka.

“Kile kilichonifanya nimtambue ni macho yake yaliyoangaza kwa umbali na bila kupoteza muda nilitoroka  kwa kasi,” alisema Bw Irungu.

Bodaboda

Wahudumu wa bodaboda nao hawajaachwa nyuma kwani wamelalamika ya kwamba ni mara nyingi wao humuona chui huyo njiani wanapowabeba wateja wao.

Naibu wa chifu wa eneo hilo la Kigumo, Bw Gatheru Mwangi alisema ya kwamba kwa muda wa  chini ya miezi miwili mbuzi kumi tayari wameuawa na chui huyo ambaye huonekana kutoka saa tatu za usiku.

Katika eneo la Maragua inadaiwa chui huyo amewajeruhi wakazi wapatao sita kwa kipindi cha miezi michache iliyopita.