Habari Mseto

Wakazi wa Murera hatarini baada ya kuharibika mfumo wa utupaji majitaka

September 21st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Murera, kaunti ndogo ya Juja, wanalalamika baada ya majitaka kuingia kwa makazi yao na maeneo ya shughuli za biashara.

Walisema Jumamosi tatizo hilo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu na hakuna hatua yoyote imechukuliwa na serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Bi Miriam Muthoni ambaye anauza chakula anasema hali imekuwa mbaya zaidi kwa sababu hata wateja wengi wamesita kuingia katika hoteli yake kutokana na harufu mbaya inayoenea mahali hapo.

“Kwa muda mrefu tumejaribu kulalamika kuhusu majitaka ya ‘sewage’ ambayo yameleta hofu ya maambukizi ya maradhi. Sasa tunaiomba serikali ya Kaunti ya Kiambu kujitokeza wazi na kutueleza ni lini wanapanga kusuluhisha tatizo hili,” alisema Bi Muthoni.

Alisema hali hiyo ni hatari kwa afya ya watoto kwa sababu kila mara wao hucheza katika maji hayo machafu bila kuelewa hatari inayowakodolea macho.

Naye Bi Tabitha Wambui ambaye ni mchuuzi wa maziwa anasema kazi yake imekuwa ngumu kwa sababu ni wateja wachache sana wanaopitia kwenye kibanda chake kununua maziwa.

Anatoa mwito kwa maafisa wa afya ya umma wajitokeze na kuhakikisha wamemaliza shida hiyo.

“Tungetaka kila mkazi wa hapa ajitahidi asafishe eneo lake badala ya kuacha maji hayo yakituama pahala pamoja,” alisema Bi Wambui.

 

Bi Tabitha Wambui, muuzaji wa maziwa katika kijiji cha Murera, Juja atoa kero yake kuhusu majitaka ya ‘sewage’ kando ya biashara yake. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema biashara nyingi mahali hapo hazipati wateja na hiyo ni hasara kubwa kwa kila mfanyabiashara.

Alisema wakati mbaya zaidi ni wa mvua ambapo maji safi huchanganyika na maji hayo machafu na baadaye huingia kwenye mabomba ya maji wanayokunywa wakazi.

Mwingine, Bi Jane Muthoni ambaye ni muuzaji wa mboga na nyanya kwenye kibanda chake alisema maji hayo yanapitia kando ya pahala pake;  jambo linaloleta utata kwa wateja wake.

“Shida tunayopitia ni kubwa kwa sababu wateja wetu hulazimika kusimama mbali wakitaka kununua vyakula. Sisi kama wakazi wa hapa tunaomba usaidizi wa haraka ili tuweze kuendesha biashara yetu kwa amani,” alisema Bi Muthoni.

Bw Isaac Kimani ambaye ni muuzaji wa viazi na kabeji alisema wamelalamika kwa muda mrefu bila jawabu lolote.

“Tunataka hatua ya haraka ichukuliwe ili sisi wafanyabiashara tuweze kuendesha shughuli zetu kwa amani. Kwa wakati huu tunahofia afya katika miili yetu,” alisema Bw Kimani.