Habari Mseto

Wakazi wa Mwakirunge kupata hatimiliki

October 19th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kisauni Ali Mbogo amewahakikishia wakazi wa Mwakirunge kwamba swala tata la ardhi litatatuliwa.

Bw Mbogo alisema Wizara ya Ardhi nchini imemhakikishia kwamba wakazi wa eneo hilo watapata hatimiliki ili kumaliza tatizo sugu la uskwota.

Hata hivyo wakazi walionywa dhidi ya kuuza vipande vya ardhi na kukosa makao.

“Usiuze shamba lako kwa sababu ujenzi wa hii barabara utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja. Lakini kila mtu atapewa hatimiliki yake kabla. Hatimiliki inafaa kuwasaidia kufanya maendeleo katika mashamba yenu ili vizazi vyenu vifaidike katika siku zijazo,” alisema Bw Mbogo.

Kadhalika alisema barabara ya Mwakirunge itakapojengwa bei ya vipande vya ardhi eneo hilo itapanda kwa faida yao.

Ingawa hivyo Bw Mbogo alisikitika kuwa wakazi wana mazoea ya kuuza mashamba kwa bei ya chini.

“Usiuze shamba kwa bei ya kutupa kama vile Sh50,000,” alionya.

Wiki iliyopita Waziri wa Ardhi Faridah Karoney ambaye alizuru eneo hilo alionya wakazi dhidi ya kuoa wake wengi pindi wanapopata hatimiliki. Badala yake aliwataka kufanya miradi ya maendeleo ili kuimarisha jamii zao.

“Ninawaomba msiuze mashamba yenu. Kuna hatimiliki nyingi sana lakini cha kusikitisha ni kuwa tukiwapatia sakabadhi hizo hapa Pwani huwa mnauza mashamba hayo baada ya miezi mitatu. Tuthamini mashamba yetu, na tuhusishe wake zetu katika maswala ya mashamba,” alisisitiza.