Wakazi wa Nyandarua waadhimisha Siku ya Punda Nchini

Wakazi wa Nyandarua waadhimisha Siku ya Punda Nchini

Na RICHARD MAOSI

WAKAZI wa eneo la Kwa Njaga, Kaunti ya Nyandarua, Jumatatu waliungana na wenzao kutoka Kisumu, Kajiado, Kitui na Nakuru kuadhimisha Siku ya Punda Nchini.

Siku yenyewe imetengwa rasmi kuangazia namna ya kumtunza punda ikizingatiwa umuhimu na thamani ya mnyama huyu kwa maisha ya binadamu.

Wakazi walichukua fursa hiyo kupanda miti na kutangamana na wataalamu kutoka Shirika la Muungano wa Wamiliki wa Punda Nchini (ADOK) ili kupokea ushauri wa jinsi ambavyo punda anastahili kutunzwa.

Mwekahazina kutoka ADOK Bi Beth Kuria, aliambia Taifa Leo, walilenga kupitisha ujumbe muhimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kumtunza punda pamoja na kumhifadhi kwenye mazingira mazuri.

Alisema wakulima wengi wamekuwa wakipitia changamoto, baada ya mifugo yao kuibwa kila kukicha hasa baada ya mahakama kuruhusu shughuli za uchinjaji wa punda kurejelewa.

“Hatua yenyewe itaendelea kumfinya mkulima kwa sababu wezi wa punda wamepata nguvu ya kuendeleza biashara haramu kwa wanunuzi, jambo ambalo litaendelea kumkandamiza mkulima,” akasema Bi Kuria.

Aidha alisema punda huchukua muda mrefu kabla ya kuzaa wakati mwingine wakifikisha hadi miaka mitatu, jambo linalowaweka kwenye hatari ya kutoweka siku za usoni endapo mikakati ya kuwalinda haitazingatiwa.

Alieleza kuwa punda wanahitaji matunzo ya hali ya juu kama vile kufanyiwa chanjo na kupatiwa dawa ya minyoo.

Shirika la ADOK lilianzisha harakati za kuwakata punda kwato na kuwashauri wakulima kuwatengenezea sehemu maalum za kukaa.

Bi Kuria alisema kuwa akina mama wengi wanaokaa mashambani, hususan wakulima, wanategemea punda kwa takriban kila kitu kama vile kusafirisha viazi kutoka mashamba yao nyumbani hadi sokoni, kubeba kuni na hata kubeba maji kutoka mtoni.

Pia mwekahazina huyo alisema wakulima wanastahili kukumbatia malisho bora kwa punda wao, badala ya kuwaacha wakijisakia malisho ya vichakani, kutibiwa na kuwakinga dhidi ya maradhi.

Vile vile alisema kuwa endapo mkulima analenga kufaidika na punda ni sharti ampatie matunzo mema.

You can share this post!

Chebukati ashuhudia maandalizi ya uchaguzi wa Juja

Tanzania: Kamati yapendekeza kuwepo kwa ‘lockdown’...