Wakazi wa Ol Moran wasita kurejea kwao

Wakazi wa Ol Moran wasita kurejea kwao

Na JAMES MURIMI

MAMIA ya wakazi wa Ol Moran, Kaunti ndogo ya Kirima, Kaunti ya Laikipia wameapa kutorejea makwao huku operesheni ikiendelea ya kuwatimua manjagili ambao wamesababisha utovu wa usalama eneo hilo.

Zaidi ya watu 330 ambao wamehepa makwao kwa hofu ya kushambuliwa, wamepiga makambi katika kituo cha ufundi cha Ol Moran huku wengi wao wakiwa wamesongwa na mawazo tele.

Mmoja wao, Bi Hannah Wambui, alihepa na familia yake kutoka kijiji cha Mirigwit baada ya majirani wake kupigwa risasi na majangili hivi majuzi.

Bi Wambui ana mvulana ambaye anafaa kufanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) katika Shule ya msingi ya Mirigwit.Mnamo Jumanne wiki jana, majangili hao walivamia shule hiyo wakati Mshirikishi wa Masuala ya Kiusalama Ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya alipokuwa akiendelea na mkutano umbali wa kilomita chache kutoka eneo hilo.

“Mtoto wangu wa kiume ni mtahiniwa wa KCPE na siwezi kumhamisha hadi shule nyingine. Nilikuwa nimeanza maandalizi ya sherehe ya kupashwa tohara kwake pamoja na kujiunga kwake katika sekondari. Yote hayo sasa yametibuka kutokana na ukosefu wa usalama,” akasema Bi Wambui.

“Hatuwezi kurejea nyumbani sasa hadi pale hofu ituondokee na masikitiko haya yaishe. Waziri Fred Matiang’i na maafisa wengine wa usalama walipotutembelea hapa, walifanya tujengeke imani kidogo ila ukosefu wa usalama bado ni changamoto kwetu,” akaongeza.

Mama huyo aliiomba serikali ijenge kituo cha polisi katika kijiji cha Mirigwit ili kukabiliana na uvamizi wa majangili. Naye, Mwalimu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Ol Moran Peris Wainaina alisema wamewapa hifadhi familia 62 ambazo zina watu 330.

Ingawa hivyo, Bi Wainaina alisema changamoto ni kuzuka kwa mkurupuko wa magonjwa yanayotokana na uchafu kwa kuwa watu hao wanatumia choo kimoja na bafu moja pekee.’Kuna tatizo la kudumisha usafi kwa sababu hatuna vyoo na bafu.

Tumekuwa tukirai familia hizo zirejee makwao kuanzia wikendi hii ila wamekataa wakihofia maisha yao,” akasema Bi Wainaina.

Mkazi Pauli Kuria naye amekuwa kambini hapo na familia yake tangu walipoamua kuondoka katika kijiji cha Mirigwit. Alisema kuwa hawezi kurejea kwake kwa sababu boma lake sasa limegeuzwa malisho ya mifugo.Zaidi ya shule saba zimefungwa huku shughuli za masomo zikilemazwa.

Juzi, watu wawili waliuawa na nyumba 50 zikateketezwa kwenye kijiji cha Kisii ndogo., siku mbili tu baada ya Bw Natembeya kuongoza mkutano katika eneo la Ol Moran.

You can share this post!

ULIMBWENDE: Njia asili za kutunza ngozi

Waislamu wakemea serikali kuhusu utekaji wa washukiwa wa...