Habari Mseto

Wakazi wa Ruiru waingiwa na hofu ya mto kuwatapikia matatizo

May 8th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

AGHALABU Mto Ruiru huwa na utulivu lakini mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika sehemu nyingi, imegeuza mkondo huo wa maji kuwa na taswira ya maporomoko ya maji.

Taifa Leo imebaini kuwa wakazi wa Gwa Kairo na Ruiru wana hofu huenda mto huo ukavunja kingo zake na kuvuruga maeneo yaliyo karibu.

“Ninaogopa kupita kwenye daraja hili sasa nikidhani huenda likaporomoka wakati wowote,” alisema Bw Daniel Irungu, mkazi wa Ruiru.

Mkazi mwingine, Bw John Mwangi anasema ni muhimu kwa wanaoishi karibu na mto huo kutafuta makazi mbadala.

“Tangu mvua ianze kunyesha, mto umevimba sana. Wanaokaa karibu na mto huu wanafaa wahame haraka na wasingoje waambiwe na serikali,” akashauri Bw Mwangi akitaja kuwa baadhi ya makazi yamejaa maji.

Waliojenga karibu na mkondo wa maji wameingiwa na wasiwasi huku Bw Mwangi akiwasihi waepuke hatari inayowakodolea macho.

Si hayo tu, wakazi wa maeneo karibu na mto huo wanahofia mlipuko wa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu.

Mabomba ya majitaka yanaonekana yamejaa pomoni mengine yakipasuliwa na maji yanayosomba kitu chochote kinachopatikana njiani.

Vilevile wakazi wanalazimika kuweka vidato vya mawe kwenye vidimbwi vya maji ili wapite huku njia nyingine zikiwa ngumu kupitika.

Wanaotumia bodaboda kadhalika hawana budi kulipa nauli maradufu, wahudumu wa pikipiki za usafiri wakiogopa maji yatawaharibia bodaboda zao.

Wahudumu wa bodaboda mjini Ruiru. PICHA | LABAAN SHABAAN