Habari Mseto

Wakazi wa Ruiru washauriwa wawe chonjo kukwepa matapeli sekta ya ardhi

August 21st, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ruiru wamehimizwa wawe chonjo wajiepushe na matapeli wa kuuza vipande hewa vya ardhi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Gathunguri Ranching Ltd, Bw John Mburu Maina amesema kuna matapeli wanaozunguka katika mji wa Ruiru wakidai wanaweza kuuza vipande vya ardhi na kutoa hatimiliki kwa wanunuzi.

“Ninawahimiza wananchi wawe makini kwa sababu lengo lao kuu ni kupotosha wananchi. Kwa hivyo, yeyote anayetaka kununua kipande cha ardhi afike ofisini kwetu ili tumsaidie kupata ardhi na cheti halali cha umiliki,” alisema Bw Maina.

Alipongeza hatua ya Waziri wa Ardhi ya kusema ya kwamba serikali itafanya kazi pamoja na kampuni za kuuza ardhi ili kuharakisha shughuli hiyo.

“Sisi maafisa wakuu katika kampuni ya Githunguri tuko tayari kabisa kushirikiana na Wizara ya Ardhi ili kufanikisha shughuli ya kuwaelekeza wanunuzi kwa wizara wapate vyeti vyao,” alisema Bw Maina.

Alisema watafanya kazi iliyo wazi kwa kila mmoja ili kila mmoja aweze kuridhika baada ya kununua kipande chake cha ardhi.

Alisema kushirikisha machifu katika zoezi hilo ni jambo muhimu na litafanikisha juhudi za serikali kuwakabidhi wananchi vyeti vyao.

Wakongwe

Mkazi mmoja wa Ruiru Bw Peter Mwaura alipendekeza serikali iwachukulie hatua kali matapeli ambao wamewalaghai wakongwe ambao hawana uwezo wa kujitetea.

“Watu wengi ambao wamepitia masaibu hayo ni wakongwe ambao wengi wao hawaelewi jinsi mambo huendeshwa. Wengi hugundua wamepoteza mamilioni ya pesa baada ya kupigwa chenga na matapeli hao,” alisema Bw Mwaura.

Bi Milka Wangui ambaye ni mkazi wa Kiang’ombe mjini Thika, alisema katika kijiji chao viwanja kadha vya shule za msingi vimenyakuliwa na matapeli.

“Sisi wakazi wa kijiji hiki tunataka serikali kuingilia kati na kuwanasa matapeli wote ambao wamehangaisha wananchi,” alisema Bi Wangui.

Alieleza kuwa wakongwe wengi wameachwa pweke baada ya matapeli hao kuwalaghai.

Alitaka serikali iwasaidie wakazi wengi ambao hawana vyeti halali wapate haraka iwezekanavyo.