Habari Mseto

Wakazi wa Sabaki wawekewa kafyu na viboko

January 18th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

WAKAZI wanaoishi karibu na mto Sabaki katika Kaunti ya Kilifi wameomba Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Nchini (KWS) kudhibiti idadi kubwa ya viboko wasumbufu.

Wengi wao wanaishi kwa woga wakihofia viboko wanaovamia mashamba yao na kuharibu mimea huenda hata wakawaumiza na kuwaua.

Jambo linalowafanya kusalia nyuma kiuchumi kwa kukodolea macho umaskini.

“Viboko wamekuwa wakihama makao yao katika fuo za mto Sabaki na kuonekana wakizurura hadi karibu na makazi ya watu,” akalalama Bw Hamisi Konga ambaye ni mkulima.

Kulingana na Bw Konga, baadhi ya wakazi wamejuruhiwa wanapokuwa wakitafuta riziki kando au karibu na mto.

Aidha ametoa onyo kwa baadhi ya vijana wanaojivinjari karibu na mto Sabaki kuchukua tahadhari ikizingatiwa kwamba hakuna uzio kuwakinga dhidi ya viboko.

Anasema wakulima wanapoenda shambani, wanalazimika kujihami kwa mapanga, mishale na marungu kwa kuhofia huenda wakavamiwa.

Isitoshe viboko wamewekea wakazi kafyu ya mchana na usiku.

Isitoshe Bi Salome Mwarua anasema wakazi wa Sabaki anasema wakazi wanalazimika kuwawekea watoto wao ulinzi mkali hasa wanapokuwa wakienda au wakitoka shuleni.

Kwingineko katika eneo la Naivasha, Kaunti ya Nakuru, wakazi wa Karagita na South Lake wakekuwa wakilalama kuhusu ongezeko la idadi ya viboko kutoka Ziwa Naivasha ambao huharibu mazao.

Aidha katika Kaunti ya Kitui kumerekodiwa visa kama hivyo ambapo wanyamapori na binadamu wamekuwa wakipigania makazi na chakula.

Hili linajiri baada ya serikali kuweka mikakati ya kuwafidia wale ambao wamewahi kujeruhiwa na wanyama wa porini.

Fidia ambayo pia inalenga kuwafikia waliobaki nyuma kama vile wajane, baada ya kufiwa na wapendwa wao.