Wakazi wa Thika wajitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Covid-19

Wakazi wa Thika wajitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Covid-19

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika walifurika kwa wingi kwenye uwanja wa michezo wa Thika ili kupokea chanjo ya Covid-19.

Zaidi ya wakazi 1,500 walipokea chanjo hiyo iliyozinduliwa na Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro.

Kulingana na gavana huyo, wamepanga kuona ya kwamba baada ya siku mbili watu zaidi ya 50,000 watakuwa wamechanjwa katika kaunti hiyo.

Alisema kwa sasa hospitali ya Tigoni Level 4 ina wagonjwa 200 waliolazwa huko kwa kuugua Covid-19.

“Kati ya hao wagonjwa, 190 wamewekwa palipo na vifaa vya oksijeni. Hata hivyo wauguzi wanaowahudumia wagonjwa hao wamejitosa kuona ya kwamba wagonjwa hao wanapona na kurejea makwao,” alifafanua Dkt Nyoro.

Alieleza kuwa tayari hospitali ya Tigoni imehifadhi vitanda 330 vya wagonjwa wa Covid-19.

Alitoa wito kwa wakazi wote wa Kiambu wapatao 2.4 milioni kujitokeza kuona ya kwamba wanapokea chanjo hiyo ili kujiweka salama.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo Dkt Joseph Murega alisema watu wapatao 14,400 wameambukizwa corona katika Kaunti ya Kiambu.

Alisema Wizara ya Afya imeweka mikakati kuona ya kwamba shughuli hiyo ya chanjo inafana.

“Ningetaka kuwahimiza wakazi wa Kiambu kufuata maagizo ya Wizara ya Afya ya kuvalia barakoa, kunawa mikono, na kuweka nafasi ya mita moja hivi kutoka kwa mmoja hadi mwingine,” alieleza Dkt Murega.

Alisema njia bora ya kujiweka salama kiafya ni kujikinga na kupata chanjo.

Alisema ifikapo mwezi Desemba 2021, wanatarajia watu asilimia 80 watakuwa tayari wamechanjwa.

Baadhi ya vituo vingine vilivyo tengwa kutoa huduma ya chanjo hiyo ni hospitali ya Munyu Health Centre, Ngoliba Health Centre, Thika Sam’s Nursing Home, na Mary Help of the Sick Hospital.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutumia vijana na wanabodaboda kuendesha kampeni...

Raila azuru TZ akiwa njiani kurejea Kenya kutoka Zambia