Habari Mseto

Wakazi waandamana wakitaka kampuni ya mawe ifungwe

January 14th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

Wakazi wa Kagoto eneo la Bahati katika kaunti ya Nakuru hapo waliandamana wikendi na kutaka kufungwa kwa kampuni moja ya upasuaji wa mawe baada ya mlipuko kutoka eneo hilo uliowaacha na hasara kubwa.

Kulingana na wakazi, mlipuko huo ulioshuhudiwa mwendo wa saa saba mchana kutoka maeneo mojawapo kampuni hiyo inapasua mawe ya ujenzi ulisababisha mtetemeko mkubwa huku baadhi ya mawe yakiharibu nyumba katika eneo hilo.

Wakazi hao waliojawa na hamaki waliifunga barabara ya Nakuru-Nyahururu wakitaka kampuni hiyo ifungwe mara moja.

Bi Rose Wairimu ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema kuwa hii sio mara ya kwanza ya tukio kama hilo kufanyika ila la hivi punde lilikuwa la kuogofya zaidi.

“Nyumba nyingi katika eneo hili zimejaa mawe ambayo yalitokana na mlipuko huo. Tunaishi kwa hofu kubwa,” alisema Bi Wairimu.

Polisi wawazuilia wakazi waliotaka kufungwa kwa kampuni ya ujenzi baada ya mlipuko uliowapa wasiwasi kutokea. Picha/ Maggy Wanja

Wakazi hao pia walisema kuwa nyumba nyingi zimejaa nyufa kutokana na mashine ambazo hutumika kupasua mawe amabazo husababisha msukosuko wa ardhi kila mara.

“Kuna watoto waliokuwa wakicheza manyumbani kwao wakati wa tukio hilo na inaogofya sana kwani mnamo mwaka 2015 tulimpoteza mtoto katika eneo hili baada ya kugongwa na jiwe kubwa kutokana ka maeneo yanayochimbwa,”alisema Bw Munyua Ndegwa, mkazi mwingine wa eneo hilo.

Meneja mmoja katika kampuni hiyo ijulikanayo kama Karsan Ramji and Sons Civil Engineering and construction Company Bi Maryline Mbaya alisema kuwa tukio hilo lilikuwa ajali.

“Hatukutarajia jambo kama hilo kwani tulikuwa tumehakikisha kuwa utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya NEMA ulifuatwa na tunaomba msamaha kwa wananchi,” alisema Bi Mbaya.

Afisa mkuu wa polisi wa ene la Bahati Bw Edward Wafula alisema kuwa shughuli katika kampuni hiyo zilisimamishwa hadi siku ya Jumatatu.

“Hakutakuwa na shughuli yoyote hadi mkutano utakaowahusisha washikadau wote kufanyika siku ya Jumatatu ambapo tutapata suluhisho ,” alisema Bw Wafula.

Mbunge wa Bahati Kimani nGunjiri pia alifika katika eneo hilo kuwatuliza wakazi hao waliojawa na hamaki.