Habari Mseto

Wakazi wabomoa kanisa, wachoma nyumba ya mhubiri

November 1st, 2018 2 min read

Na CHARLES LWANGA

WAKAZI wa Bungale eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi wamebomoa kanisa linalohusishwa na pasta mwenye utata ambaye hueneza injili kupitia kwa runinga, Bw Paul Makenzi.

Pia walichoma nyumba ya mhubiri wa kanisa hilo la Good News International, Bw Titus Katana iliyojengwa takriban mita 50 kutoka kanisa hilo kwa madai kuwa anaeneza mafunzo ya uongo kuhusiana na Ukristo.

Naibu Kamishna wa Magarini, Bw Simon Lokorio alithibithisha tukio hilo akisema kuwa wakazi waliojaa hasira waliandamana kabla ya kubomoa kanisa hilo Jumapili jioni wakidai kuwa linaeneza itikadi kali.

Bw Lokorio alisema anafuatilia tukio hilo huku akidai alikuwa amemuonya Bw Katana asirudi eneo hilo hadi wakati hali ya taharuki itakapoisha.

“Lakini alirudi huko na kuanza kuunda kanisa hilo ambalo lilikuwa limebomolewa licha ya kumuonya kuwa wakazi waliokasirishwa na mahubiri yake wanataka kanisa hilo lifungwe,” alisema.

Bw Rogers Kalama, mkazi wa eneo hilo alisema waliandamana wakati mhubiri alianza kukashifu elimu na matibabu ya hospitalini.

“Tuliandamana alipoanza kuhubiri kuwa elimu ni ovu na haina msingi wa kidini kulingana na Biblia,” alisema akiongeza pia alifundisha kuwa watu wanafaa wategemee Mungu pekee kupata matibabu.

Bw Katana ambaye pamoja na familia yake wametorokea mjini Malindi alisema wamepata hasara ya Sh2.5 milioni baada ya kuchomewa nyumba na kanisa.

Akizungumza na wanahabari katika kanisa la Good News International ambapo aliambatana na bibiye Agnes Nzai na Kasisi Makenzi, alisingizia viongozi wa serikali kwa kuchochea wakazi ili kuchoma nyumba yao.

“Wazee wa vijiji na Nyumba Kumi wakishirikiana na naibu wa chifu walidai kuwa ninahubiri mafunzo ya uwongo na wakataka kanisa hilo lifungwe,” alisema na kuongeza kuwa “chifu wa eneo hilo pia amekuwa akiedeleza uchochezi kwa baraza na mikutano za hadhara.”

Bw Katana ambaye alihadhitia jinsi amewai kutiwa mbaroni kwa ‘kuhubiri neno la Mungu’ aliuliza ni kwa nini serikali haikuchukuwa hatua ya kulinda mali yao.

“Saa hizi sisi ni wakimbizi wenye hawana makao licha ya kuwa na boma na kanisa eneo la Bungale,” alisema na kuongeza “vipasha sauti, nguo na viti ziliharibiwa ndani ya nyumba na kanisani.”

Bw Katana alisema waumini wake sasa wanaishi kwa wasiwasi wa kuvamiwa na wakazi kwani mkono wa serikali umeonekana wazi katika kisa hicho ambacho kimewawacha maskini.

Bibiye ambaye ni mjamzito alisema maafisa wa polisi wamewashika waumini mara kadha wakiwa kanisani na kuwazuia katika kituo cha polisi cha Marereni.

“Tumeshikwa mara nyingi na kuwachiliwa bila mashtaka lakini hatuelewi ni kwa nini bado hawajashika watu waliotuchomea nyumba,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Makenzi alikashifu maafisa wa serikali na wanasiasa kwa kuchochea watu kuvamia kanisa lake wakati kesi inaendelea kortini.

“Ni jambo la kushangaza kuwa maafisa wa serikali wanaambia watu wafuate sheria za nchi wakati wenyewe wanaongoza wakazi kuvamia na kubomoa mali binafsi kinyume na sheria,” alisema.

Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, maafisa wa polisi walivamia kanisa lake na kuokoa watoto 93 na kumshika Bw Makenzi na baadhi ya wafuasi wake.

Alishtakiwa kwa kosa la kueneza itikadhi kali, kufundisha kwa shule iliyokuwa haijasajiliwa serikalini na kumyima mwanawe haki ya masomo.

Alikata mashtaka hayo na akawachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi hicho.