Habari Mseto

Wakazi wachoma nyumba sita za mshukiwa wa uchawi

February 13th, 2019 1 min read

Na GEORGE ODIWUOR

POLISI katika eneo la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay walikuwa na wakati mgumu kutuliza wanakijiji waliochoma nyumba sita wakidai mwenyewe ni mchawi.

Wakazi wa kijiji cha Rachong’, Kata ya Kubuoch Magharibi, walimshambulia Mzee Gabriel Osaso, mwenye umri wa miaka 79, kwa madai kwamba alihusika katika kifo cha mwanafunzi wa Darasa la Kwanza mnamo Ijumaa.

Mzee Osaso alilaumiwa kuwa mchawi kwenye harakati za kutafuta mwili wa Veronicah Achieng’, aliyekuwa mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Ombo.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa na mamba katika Mto Kuja.

Wanakijiji hao walisema mshukiwa alisikika akisema kwamba mwili wa marehemu haungepatikana baada yake kuufanyia mazingaombwe.

Chifu wa eneo hilo, Joseph Ogur alisema polisi walilazimika kumwokoa mzee huyo kutoka kwa umati huo ambao ulitaka kumdhuru.

Mnamo Jumapili, wanakijiji walichoma nyumba sita katika boma la mzee huyo na vitu vyote vilivyokuwa ndani.