Habari Mseto

Wakazi wafurahia ujenzi wa barabara

December 16th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ngoingwa wamepongeza juhudi za KeNHA kukarabati barabara ya Mang’u-Ngoingwa kutoka kwenye barabara kuu ya Thika Super Highway.

Barabara hiyo kuu aina ya Dual-Carriage inayounganisha ile ya Njomoko ikielekea Ngoingwa hadi Mang’u, na Gatundu Kaskazini ni ya kilomita 14.

Wakazi hao walisema biashara yao itaimarika pakubwa kutokana na ukarabati wa barabara hiyo inayotarajiwa kukamilika baada ya miezi michache.

Bw John Mwangi ambaye ni mwakilishi wa mbunge wa Thika, alisema hiyo ni hatua kubwa kwa wakazi hao ambao kwa muda mrefu wametamani kuwa na barabara nzuri eneo hilo.

“Tuna matumaini ya kwamba barabara ya hali ya juu itaundwa sehemu hiyo na wananchi watanufaika pakubwa kwa sababu biashara yao itaimarika,” alisema Bw Mwangi.

Alisema kwa muda mrefu barabara inayotumika kwa sasa ni mbovu na magari mengi yamekuwa yakikwama yanaposafirisha bidhaa sehemu tofauti.

Maafisa wa kutoka afisi ya KeNHA walizuru eneo la Ngoingwa mwishoni mwa wiki ili kupata maoni tofauti ya wananchi kuhusu barabara hiyo inayotarajiwa kujengwa mara moja.

Wakazi hao walihakikishiwa kuwa yeyote atakayeathiriwa na mpango huo atalipwa ridhaa bila wasiwasi wowote.

Baada ya barabara hiyo kukamilika itapunguza msongamano wa magari ambayo imekuwa ikishuhudiwa kila mara.

Wakazi hao pia walihakikishiwa kuwa mabomba ya kusafirisha maji taka yatawekwa ili kuzuia mafuriko ya kila mara inayoshuhudiwa kukinyesha.

Bi Jane Njeri mkazi wa eneo hilo alisema Halmashauri hiyo ya KeNHA inastahili kuajiri wakazi wa hapa karibu ili vijana nao wanufaike kwa ajira.

Wengi wa wakazi wa Ngoingwa walikubaliana na pendekezo hilo wakisema ni njia moja ya kuwaepusha vijana wengi kutoingilia maovu mitaani.