Habari Mseto

Wakazi wahamishwa tayari kuanza mradi wa maji wa Kariminu 2 Dam

April 4th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE  ONGARO

MRADI wa maji wa Kariminu 2 Dam eneo la Gatundu Kaskazini tayari umeanza kutekelezwa rasmi baada ya wakazi wengi kuhamishwa kutoka eneo hilo.

Mhandisi wa kampuni ya maji ya Athi Water Service Bw Michael Thuita, alisema kampuni ya Avic International Holding Co-Operation, na ile ya Shangai Municipal Engineering Design Institute zimepewa kandarasi hiyo ambapo tayari vifaa vya ujenzi vimepelekwa mahali hapo.

Makandarasi walitia saini kandarasi ya mradi huo miaka miwili iliyopita ambapo awamu ya kwanza itazinduliwa katika eneo la Buchuna, Gatundu Kaskazini.

Bw Thuita alisema ya kwamba familia zipatazo 93 zimepokea fidia zao huku wakijitolea kuacha ardhi yao ya takribani ekari 47.

Mradi huo ulikuwa umetarajiwa kuzinduliwa miaka minane iliyopita ambapo kitita cha Sh 4.7 bilioni zilitolewa wakati wa makubaliano ya pande mbili.

Alisema mradi huo ukikamilika utagharimu takribani Sh 24 bilioni, huku huduma ikitolewa katika maeneo ya Gatundu Kusini, Juja, Ruiru, na maeneo ya Nairobi na sungosungo zake.

Miezi sita

Alieleza ya kwamba wakazi wote waliopokea fidia zao wamepewa muda wa miezi sita hivi wawe wamepata mahali tofauti pa kwenda kuishi.

“Tunatarajia kazi hiyo ikiendeshwa vyema bila kutokea matatizo yoyote itakamilika baada ya miaka mitatu hivi,” alisema Bw Thuita.

Alisema hata ingawa kuna wakazi wachache ambao hawajalipwa fedha zao za fidia lakini wanatarajia shughuli hiyo itakamilika baada ya wiki moja hivi ili eneo hilo liwe wazi kabisa kwa mradi huo kuendeshwa bila shida.

“Tungetaka kuona ya kwamba kila mkazi anapata haki yake na anajitafutia makao yake popote apendapo bila kushurutishwa  kwa vyovyote vile,” alisema Bw Thuita.

Alisema kuchelewa kwa kuzinduliwa kwa mradi huo ilikuwa kwa sababu ya mivutano ya maswala ya ardhi katika eneo hilo na kwa hivyo ilibidi kila kitu kuchunguzwa kwa umakinifu.

Alisema kulingana na mipango iliyoko eneo hilo litachimbwa na kuweka bomba kubwa la maji litakalosafirisha maji hadi eneo la kuyasafisha ili yaweze kusambazwa katika miji tofauti katika Kaunti ya Kiambu na vitongoji vyake.