Wakazi wakeketwa na njaa mifugo ikizidi kuangamia

Wakazi wakeketwa na njaa mifugo ikizidi kuangamia

Na WAANDISHI WETU

FAMILIA katika kaunti zinazokumbwa na ukame zinaendelea kuathiriwa na njaa na kiu tangu Rais Uhuru Kenyatta atangaze ukame janga la kitaifa mnamo Septemba.

Wakazi kutoka kaunti hizo wanalalamika kuchelewa kwa serikali kutimiza ahadi yake ya kuwalinda dhidi ya janga hilo kwa kununua na kuwatafutia soko mifugo ili kupunguza hasara za ukame.

Hadi sasa, serikali haijaanza mchakato huo Kaunti ya Samburu, jambo linalowatia wasiwasi wafugaji.

Wakazi wa Kaunti ya Samburu wanalalamika kuchelewa kwa serikali kununua na kutafutia soko mifugo yao baadhi ya wanyama hao wa kufugwa wakiendelea kufa.

“Baadhi ya ng’ombe, kondoo, mbuzi na ngamia wamelemewa na ukame. Kwa sasa, bei yao imepungua. Tunapata hasara sana kama wafugaji. Tunaomba serikali ifanye hima ili kuokoa mifugo wetu,” akasema Bw Julius Leokono, mmoja wa wafugaji.

Wafugaji hao wanasema wameshindwa kupata karo na hata pesa za kujikimu kutokana na athari za ukame.

Kulingana na Mamlaka inayosimamia ukame (NDMA), bei ya mifugo inaendelea kushuka kutokana na hali duni ya kiafya inayosababishwa na ukosefu wa lishe na maji.

Kwingineko, maelfu ya watoto Kaskazini mwa Kenya wanakumbwa na utapiamlo kutokana na ukame unaoshuhudiwa katika maeneo hayo.Wakenya milioni 2.5 wameathiriwa na janga hilo huku baadhi yao wakikosa chakula na maji.

Kulingana na ripoti ya wizara ya Afya na Kilimo, Wakenya wengi bado wataendelea kuathiriwa na ukame na utapiamlo.

“Zaidi ya watoto 10,000 Kaunti ya Turkana na akina mama 6,000 wana utapiamlo. Hii ni kwa sababu gharama ya maisha imepanda,” inasoma ripoti.

Katika kaunti ya Meru wakazi zaidi ya 120,000 wanahitaji msaada wa chakula kwa dharura kutokana na ukame ambao umekuwa ukihangaisha eneo hilo.

Kamishna wa Meru, Karuku Ngumo, alitaja maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame kama Igembe na Tigania ambapo mvua imekosa kunyesha kwa miaka miwili.Kulingana na NDMA, mazao katika eneo la Meru yalikuwa duni msimu uliopita huku baadhi ya maeneo yakikosa kuvuna chochote.

Katika Kaunti ya Kilifi, serikali imeanza kugawa chakula cha msaada kwa wakazi wanaoathiriwa na ukame.

Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa alizindua shughuli hiyo katika vijiji vya Chakama na Bofu eneobunge la Magarini.

Wamalwa alisema kwamba chakula hicho kitasambazwa maeneo ya Pwani, Kaskazini Mashariki na Rift Valley ambako wakazi wameathiriwa na ukame.

Nalo Shirika la Msalaba Mwekundu limeanza kutoa msaada wa chakula na fedha kwa familia kutoka Kaunti za Turkana, Pokot Magharibi na Baringo.

Ripoti za Geoffrey Ondieki, Barnabas Bii, Sammy Lutta, David Muchui na Maureen Ongala

You can share this post!

Raila kukita kambi ngome yake Ruto

Ngilu aagizwa afike kortini kueleza sababu ya kutolipa...