Wakazi walaani polisi kuwatesa Mama Ngina

Wakazi walaani polisi kuwatesa Mama Ngina

Na MOHAMED AHMED

WAKUU wa polisi wanachunguza malalamishi kuwa maafisa wa usalama wana tabia ya kuwahangaisha raia wanaoenda kubarizi katika Bustani ya Mama Ngina, Kaunti ya Mombasa kwa nia ya kula hongo.

Bustani ya Mama Ngina imekuwa ikiendelea kupata sifa kwa muda sasa baada ya serikali kutumia zaidi ya Sh400 milioni kuipa mvuto mpya.

Kubadilishwa kwa taswira ya bustani hiyo kumepelekea kuongezeka kwa Wakenya wanaofika hapo kubarizi.Hata hivyo, licha ya upepo mwanana unaopatikana kwenye bustani hiyo kutokana na ukaribu wake na bahari, maafisa wa usalama wamekuwa kero kubwa.

Kwa muda sasa, Taifa Leo imekuwa ikifuatilia maafisa hao ambao wanalenga kuchukua hongo kwa wageni na wakazi wa Mombasa ambao humiminika sehemu hiyo hususan siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Kulingana na uchunguzi wetu wa kina, maafisa hao hutumia tuktuk kushika doria eneo hilo na hulenga kuwahangaisha wanaume na wanawake ambao hutembea pamoja katika bustani.

Maafisa hao huwashika watu hao kwa madai ya kuwa wanafanya mapenzi hadharani na kuwataka watoe pesa ndipo waweze kuachiliwa.Katika kisa cha hivi majuzi ambacho kimeibua hisia kali miongoni mwa wakazi, maafisa wawili walimkamata kijana wa mkazi mmoja eneo la Mombasa.

Wakazi waliokuwa hapo na kushuhudia kisa hicho walisema kijana huyo alikuwa amekaa ndani ya gari lake.Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binadamu Khelef Khalifa aliwalaumu maafisa wa usalama kwa kunyanyasa watu.

‘Maafisa wa polisi wanawanyanyasa watu kwa kuwashika bila makosa ya kisheria na kisha kuchukua pesa kutoka kwao. Kwanzia lini maafisa wa usalama wamepewa jukumu la kuangalia tabia za kibinafsi za watu?’ akauliza Bw Khalifa.

Bw Khalifa alimtaka kamanda wa polisi eneo la Pwani Gabriel Musau kuwachukulia hatua maafisa hao.Bw Musau kwa upande wake alisema kuwa kisa hicho kinachunguzwa na kuahidi kuwa mlalamishi wa kisa cha hivi juzi amekuwa akijulishwa kuhusiana na uchunguzi huo. ? ‘Suala hili linashughulikiwa vilivyo,’ akasema Bw Musau.

You can share this post!

BURUDANI: Angie The Twerker ni mwigizaji mwenye talanta ya...

Wanaolengwa na chanjo ya crorona waingiwa na hofu