Habari MsetoKimataifa

Wakazi walalama bidhaa za Tanzania kujaa sokoni mwao na kuvuruga biashara

November 1st, 2018 2 min read

Na LUCY MKANYIKA

WAFANYABIASHARA wa Taveta, mpakani mwa Kenya na Tanzania wanalamikia kujaa kwa bidhaa za Tanzania katika soko lao.

Wafanyabiashara hao walisema kuwa bidhaa kutoka Tanzania zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya chini mno na hivyo kuharibu soko la mali yao.

Akiongea sokoni humo, Bi Lucy Mwikali alisema kuwa serikali imewapa nafasi wafanyabiashara wa nchi hiyo jirani kufanya biashara huru nchini Kenya ilihali wao hawaruhusiwi kufanya biashara Tanzania.

“Bei ya ndizi imeshuka kwa kuwa wenzetu wanakuja na malori yamejaa mizigo. Sisi ambao tunauza rejareja tunapata hasara,” akasema Bi Mwikali.

Alisema kuwa wateja hupendelea mali ya Watanzania kwa kuwa bei yao ni ya chini mno.

“Kwanza tunauza hasara, pili kupata wateja imekuwa vigumu kwa kuwa bei yetu ni ya juu tukilinganisha na ya wenzetu,” akasema.

Bw Philip Kandia alisema kuwa ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki haujafaidi Wakenya.

Bw Kandia alieleza kuwa mkataba wa soko huru kwa nchi mwanachama haujatekelezwa na nchi ya Tanzania na hivyo kuhujumu mchakato wa kufanya biashara huru.

“Sisi Wakenya haturuhusiwi kabisa kuuza bidhaa zetu Tanzania. Ukijaribu utashikwa na bidhaa zako kufichwa,” akasema.

Alisema ipo haja ya serikali kulinda wafanyakazi wake kutokana na maonevu ya kibiashara kati yao na majirani wao.

Alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kutoa nchi ya Kenya kutoka kwa mwafaka wa makubaliano na nchi ya Tanzania ikiwa wataendelea kuwakataza Wakenya kufanya biashara nchini humo.

Hata hivyo, Naibu Gavana wa kaunti hiyo, Bi Majala Mlaghui aliwataka wenyeji kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu za kibiashara za nchi za nje.

Alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo itahakikisha kuwa inaungana na wizara ya biashara ili kuhakikisha wanapata soko za nje za bidhaa zao.

Aliwataka wafanyibiashara hao vilevile kuchukua nafasi za biashara za Comesa, Igad na zingine badala ya kuzingatia zile za Afrika Mashariki pekee.

“Kuna nafasi nyingi sana za biashara za nchi za ng’ambo mbali na hii ya majirani wetu Watanzania,” akasema.