Wakazi walalamika unyakuzi bandarini

Wakazi walalamika unyakuzi bandarini

Na KALUME KAZUNGU

WAMILIKI wa ardhi zinazopakana na Bandari ya Lamu wameomba uchunguzi uanzishwe kuhusu unyakuzi wa ardhi za kijamii.

Wakazi hao wamewasilisha malalamishi kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kwamba kuna mabwanyenye wanaonyakua ardhi zao za kijamii.Wamiliki hao chini ya Muungano wa Wakulima wa Kililana (KFO), wanadai zaidi ya ekari 5,000 za ardhi tayari imenyakuliwa maeneo ya Kililana na Mashunduani na mabwanyenye hao, wanaodaiwa wana hatimiliki bandia.

Msemaji wao Bw Mohamed Rajab alihoji kuwa baadhi ya mabwanyenye wanaohusika ni maafisa wakuu serikalini.Tandabelua la umiliki limeandama mashamba hayo kwani endapo wamiliki watalazimika kuhama, serikali itahitajika kuwalipa mamilioni ya pesa kama fidia.

Vilevile, sehemu za ardhi hizo zinatarajiwa kuvutia waekezaji ambao wanataka kufungua biashara za bandarini, na hivyo inatarajiwa kuwa bei ya ununuzi ardhi itapanda mno.Mnamo Februari 2015, serikali ya kitaifa ilitoa Sh1.3 bilioni na kukabidhi Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ili kuwafidia wamiliki wa ardhi ya ekari 70,000 zilizotwaliwa kwa ujenzi wa Bandari ya Lamu.

Bw Rajab alifichua kuwa kati ya ekari 5,000 wanazolalamikia, tayari 2,500 zimejumuishwa kwenye ardhi hiyo ya ekari 70,000 ya bandari ilhali wamiliki halisi hawajafidiwa.“Waliofidiwa ni wengine ilhali wale tuliostahili tumeachwa kuteseka.

Tunataka haki yetu,” akasema Bw Rajab.Mzee wa kijiji cha Kililana, Bw Kombo Abushir, alishangaa kwanini serikali imekuwa ikiwachenga wamiliki halisi wa ardhi hizo badala ya kuhakikisha wamepewa hatimiliki ili zisinyakuliwe.

“Tunashangaa jinsi hawa mabwanyenye wanavyojigamba kuwa na hatimiliki za ardhi ambazo tumeishi hapo kwa zaidi ya miaka 30. Tuko na makaburi, visima na misikiti ya tangu mababu zetu. Tumepanda miti ya kale kwenye ardhi hizo kuashiria kuwa sisi ndio tumeishi pale maisha yetu yote.

“Inakuwaje leo hii mtu anajitokeza kudai ndiye mmiliki halisi wa ardhi zetu? EACC na DCI ichunguze na kuwakamata hawa wanaoendeleza unyakuzi wa ardhi zetu Lamu,” alieleza Bw Abushir.Naye Bi Mwanamina Amin aliongeza kuwa mbali na ardhi zinazopakana na bandari, hata vipande vidogo vya mashamba waliyobakishiwa pia vinaandamwa na matajiri hao.

“Tutasimama kidete kutetea ardhi zetu hadi haki ipatikane. Serikali ina jukumu la kuhakikisha wamiliki wote halisi wa ekari 70,000 ilizotwaa wanalipwa fidia yao ili watafute makao mbadala,” akasema.Suala la umiliki wa ardhi limekuwa donda sugu katika maeneo ya Pwani kwa miaka mingi.

Licha ya serikali kusema imepiga hatua kubwa kuwapa wenyeji hatimiliki, baadhi ya viongozi wanasisitiza kuwa nyingi ya hati hizo zinapeanwa katika maeneo ambako hakuna mizozo mikubwa, hususan maeneo yanayovutia uwekezaji wa miradi mikubwa na biashara kama mradi huo wa Bandari ya Lamu.

You can share this post!

Wasimulia jinsi walikaa shimoni siku 7 bila chakula

Wanajeshi wa Ulinzi Warriors watupia jicho Ferroviario...

T L