Wakazi walia barabara mbovu zinawaletea hasara

Wakazi walia barabara mbovu zinawaletea hasara

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa mtaa wa Zimmerman, Nairobi wanalalamikia muundomsingi duni wa barabara eneo hilo, wakilia sasa wanapata hasara kwa biashara. Wanasema nyingi ya barabara ni mbovu na zinaendelea kuchakaa mvua inapozidi kushuhudiwa.

Kaunti ya Nairobi imekuwa ikishuhudia mvua kipindi cha muda wa siku chache zilizopita.

“Barabara za mtaa huu zinaendelea kuwa mbovu, hazipitiki hasa kipindi hiki cha mvua. Kama una biashara eneo hili, basi wateja wanakuhepa, wanaenda kununu bidhaa maeneo ambayo barabara ina lami. Hali hii imeniletea hasara,” akateta Bw Simon Muchiri, mkazi.

Taifa Leo Dijitali imefanya ziara eneo hilo na kubaini barabara kadha zinaendelea kuharibika.

“Tumekuwa tukijaribu kuhimiza viongozi eneo hili watuimarishie, ila wameendelea kutupuuza. Barabara unazoona zimeharibika kupita kiasi zimesalia hivyo kwa zaidi ya miaka mitano. wakati mwingine magari yakakwama na kuchelewesha bidhaa,” akasema mkazi mwingine.

Zimmerman ni kati ya mitaa yenye idadi ya juu ya watu Kaunti ya Nairobi.

Ni barabara chache pekee, ikiwemo ile ya Base inayoonekana kushughulikiwa. Imeunganishwa na Kamiti Road kwa matofali maalum aina ya cabros.

Huku nyingi ya barabara za mashinani na mitaa ikiwa jukumu la serikali za kaunti kuziimarisha, wenyeji wanawaomba viongozi wa kisiasa eneo hilo kuangazia changamoto za usafiri na kutembea wanazopitia.

You can share this post!

Familia 3,000 zaagizwa kuhama Mto Ngong

Wanahabari wa spoti wa NMG watwaa tuzo