Habari Mseto

Wakazi walia kero la kunguni Mombasa

January 16th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

WAKAZI katika baadhi ya mitaa Kaunti ya Mombasa, wanahangaika baada ya kunguni kufurika manyumbani mwao na magari ya matatu.

Wadudu hao ambao hunyonya damu na kutoa harufu mbaya, wanatesa zaidi wakazi wa mitaa ya Mishomoroni, Tudor na Likoni kando na kupenya pia katika magari ya uchukuzi wa umma.

Bw George Kamau, mmoja wa wakazi, alisema amelazimika kunyunyuzia nyumba yake dawa ya kuwaua wadudu hao mara tatu kila mwezi ili kuhakikisha hawaongezeki.

“Kama uko Mombasa na hujawahi kuumwa na kunguni basi hujakaribishwa katika mji huu. Kunguni wako katika nyumba nyingi, katika magari na tunastaajabu sana kwani imekuwa vigumu sana kuwamaliza,” alisema Bw Kamau.

“Ukinyunyiza dawa kwako na majirani wako hawajafanya hivyo, basi kuna uwezekano kunguni watarudi katika nyumba yako tena baadaye,” akasema.

Mkaazi mwingine, Evelyne Wakesho alisema licha ya kutumia mbinu tofauti, bado ilikuwa vigumu kuwaua kunguni walioingia kwake.

Alisema alitumia maji moto, akaanika malazi kwenye jua kila siku ya wiki na kunyunyiza dawa chumbani mara tatu kwa wiki kabla ya kwenda kazini lakini bado ikawa vigumu kuwaua.

“Wadudu hawa wakivamia nyumba yako huwa hatari sana kwa vile itakuwa vigumu kuwamaliza,” akasema Bi Wakesho.

Bw Francis Kimani, ambaye hufanya kazi ya kunyunyiza dawa za kunguni, alisema amepata wateja wengi sana katika maeneo ya Mishomoroni, Tudor na Likoni.

Dkt Levin Shikanda kutoka hospitali ya Al- Farooq, Mombasa alisema mng’ato wa kunguni huwa unaweza kusababisha maradhi na kuharibifu ngozi.

Msemaji wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Bw Richard Chacha alieleza kuwa unyunyizaji wa dawa katika nyumba zilizoathirika utapewa kipaumbele maafisa wa afya wakithibitisha hali hiyo ni mbaya.