Habari Mseto

Wakazi walia nzige wamekula mimea inayoota msimu wa upanzi

April 20th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Uwepo wa nzige katika kaunti ya Samburu unazidi kuzua tumbo joto miongini mwa wakulima hata baada ya mvua ya upanzi kunyesha.

Taifa Leo imebaini kuwa wakulima wengi katika kaunti hiyo kwa sasa wanahofia kuwa nzige hawa huenda wakamaliza mimea inayoota.

Kundi la nzige limeonekana maeneo ya Porro, Baawa na Laparta, maeneo ambayo upanzi unaendelea.

Maeneo mengine ambayo yameathirika na uvamizi wa nzige ni pamoja Wadi ya Ndoto na North Horr.

Elizabeth Lesegwe, mkulima kutoka maeneo ya Porro alielezea wasiwasi wake kuwa wadudu hao hatari huenda wakafagia shamba lote la mboga na mahindi iwapo mbegu alizopanda siku nne zilizopita zitaota.

Bi Lesegwe ambaye pia amepanda maharagwe alisema anahofia kuvuna hasara kutokana na uwepo wa nzige hao.

“Tulikuwa na matumaini kuwa serikali itamudu kuwamaliza nzige hawa kabla mvua ya upanzi kurejea. Mimea yetu haiko salama. Mahindi niliyopanda imekaribia kuota wakati wowote kutoka sasa na iwapo nzige watavamia basi familia yangu iko matatani,” alisema Bi Lesegwe.

Aliomba serikali kuu na ile ya kaunti kuangamiza nzige ambao wamepiga kampi katika kaunti ya Samburu kwa muda sasa.

Moses Lekenit, ambaye pia ni mkulima alikiri kuwa kupanda mimea kwa sasa ni kama ‘kuzika raslimali’. Alisema kuwa nzige ni tishio la usalama wa chakula katika kaunti hiyo.

“Hatujaona hatua kubwa ambayo imepigwa na serikali katika kupigana na nzige. Tunahofia kukosa chakula ikizingatiwa pia uwepo wa virusi vya Corona,” alisema.

Hata hivyo, afisa mkuu wa programu maalum Daniel Lesaigor alikiri kuwa nzige ambao wamevamia mashamba katika eneo la Samburu ya Kati huenda ikamaliza Miche yote wakati upanzi utakamilika.

“Ni wakati upanzi an nzige wameenea mpaka Samburu ya Kati. Wakulima Wana kila sababu ya kuhofia lakini tunafanya kila juhudi kuwaangamiza,” aliongeza.

Bw Lesaigor alisema kuwa juhudi za kumaliza nzige hao zimelemazwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa katika kaunti ya Samburu.

“Mvua imeleta changamoto kwa siku nne zilizopita. Tunaponyunyiza dawa kutoka angani mvua huosha yote,” alisema Bw Lesaigor.