Habari Mseto

Wakazi walia vibanda vya video vinawaharibia watoto

March 26th, 2020 1 min read

Na TITUS OMINDE

WAZAZI na walezi mjini Eldoret wanataka serikali ivifunge vyumba vyote vya kuonyesha video.

Wanasema vyumba hivyo vinaruhusu watoto kutumia wakati wao mwingi kwenye kumbi hizo wakati huu wanapokuwa nyumbani kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

Wazazi kutoka maeneo ambayo biashara ya video inazidi kuongezeka walidai kuwa wamiliki wa video hizo wanatumia athari ya ugonjwa wa Covid-19 kwa shule kupata pesa za ziada kutoka kwa watoto walio nyumbani.

“Kwa takribani wiki moja ambayo watoto wamekuwa nyumbani kwa sababu ya virusi, wamegeuza kumbi za video kuwa shule. Tunataka serikali kuingilia kati na kufunga kumbi hizi kwa kuruhusu watoto wetu kushinda huko,” alisema Bi Maureen Akinyi, mmoja wa wazazi kutoka mtaa wa Langas.

Bi Akinyi aliongeza kuwa kumbi hizo hazizingatii masharti ya usafi ikizingatiwa kuwa kuna msongamano katika kumbi hizo.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo mtaani Langas ulibaini kuwa ni biashara kama kawaida mtaani humo bila kujali maagizo ya serikali kuhusu virusi hivyo.

Hali ni sawa na hiyo katika mitaa ya Kamukunji, Munyaka, Huruma kati ya makazi mengine katika mji wa Eldoret.

Gavana Jackson Mandago hapo awali alielekeza maeneo yote ya burudani yafungwe.Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Bw Johnstone Ipara alisema maafisa wake watashika doria mitaani, baada ya baadhi ya wakazi kukataa kukaa ndani ya nyumba zao.

“Wakazi wote ni lazima wasalie ndani, isipokuwa kusafiri kwenda mjini kwa ununuzi wa chakula au kutafuta huduma ya matibabu,” akasema.