Habari za Kaunti

Wakazi wamtetea Natembeya, wamkosoa seneta Chesang kwa kumshambulia

May 14th, 2024 2 min read

NA EVANS JAOLA

BAADHI ya wakazi wa Trans Nzoia wanamtetea Gavana George Natembeya dhidi ya mashambulizi kutoka kwa viongozi wa Kenya Kwanza huku joto la kisiasa likiendelea kupanda katika kaunti hiyo.

Tofauti za kisiasa za hivi majuzi kati ya Natembeya na Seneta Allan Chesang zimesababisha joto la kisiasa kupanda katika kaunti hiyo baada ya seneta huyo kumlaumu Natembeya kwa madai ya kutosimamia vyema pesa za kaunti na utekelezaji wa miradi ya kaunti.

Hatua hiyo inajiri baada ya Seneta Chesang kumlaumu Natembeya kwa kutenga viongozi wengine waliochaguliwa wa kaunti hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kutoa msaada wa chakula kwa waathiriwa wa mafuriko katika eneo la Namanjalala kaunti ndogo ya Kwanza Jumamosi iliyopita, Seneta Chesang alihoji jinsi pesa za miradi ya kaunti zinavyotumiwa na kumtaka Gavana Natembeya kutoa maelezo kuhusu pesa hizo.

Seneta huyo amekuwa akidai pesa za kaunti zinatumiwa vibaya kupitia miradi ya ruzuku kama usambazaji wa mbegu za mahindi kwa wakazi.

Chesang pia alilalamika kuhusu madai ya ukosefu wa dawa katika vituo vya afya katika kaunti hiyo na kumtaka Gavana Natembeya kukubali kwamba ameshindwa kusimamia kaunti.

Vile vile, amekuwa akimlaumu gavana huyo kwa kutochukua simu zake na kutojibu maswali kuhusu matumizi ya pesa anayoulizwa na afisi yake.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wamemlaumu seneta huyo kwa kutoa vitisho na na kupanga kumchafulia jina Gavana Natembeya.

Wakazi hao walisema kwamba mashambulizi ya kisiasa dhidi ya Gavana Natembeya kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza katika kaunti hiyo yanalengwa kuhujumu juhudi zake za kubadilisha uongozi eneo la Magharibi.

Wakazi hao walimuonya seneta dhidi ya kutumia jukumu lake la kumulika usimamizi wa kaunti kutimiza maslahi ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Iwapo seneta ana masuala ya kulalamikia anapaswa kufanya hivyo katika seneti na gavana aitwe kujibu lakini hatutamruhusu afanye siasa duni kumhujumu gavana,” alisema Bw Peter Wafula mkazi wa kaunti ndogo ya Kwanza.

Bi Mary Chemtai, mkazi wa eneobunge la Cherangany alisema wako na imani na gavana wao na mashambulizi dhidi yake yananuiwa kumsumbua akose kufanya kazi ya kuleta maendeleo katika kaunti yao.

Madiwani wa kaunti hiyo nao wakiongozwa na naibu kiranja wa wengi aliye MCA wa wadi ya Kapomboi Kepha Were walisema kuwa seneta Chesang amekuwa wa kueneza uvumi na kusababisha migawanyiko kati ya viongozi wa kaunti.