Wakazi wanung’unika baada ya Ruto kuteua mwaniaji kiti Mathira

Wakazi wanung’unika baada ya Ruto kuteua mwaniaji kiti Mathira

NA STEPHEN MUNYIRI

BAADA ya kumteua Rigathi Gachagua kuwa mgombeaji mwenza wake, Naibu Rais William Ruto wikendi alimuidhinisha diwani Eric Mwangi Wamumbi kugombea ubunge wa Mathira kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA).

Dkt Ruto alimtambulisha diwani huyo wa Konyu katika mkutano wa kisiasa mjini Karatina mnamo Jumamosi alipokuwa akizuru kaunti hiyo kujipigia debe kwa mara ya kwanza tangu amteue Bw Gachagua.

Hata hivyo, umati haukupokea vyema uamuzi huo huku baadhi wakimzomea Dkt Ruto baada ya kutoa tangazo hilo.

Wiki jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa UDA, Anthony Mwaura alitangaza kuwa wale ambao wangependa kupata tikiti ya chama hicho watume maombi.

Wananchi waliozungumza na Taifa Leo nao walisema diwani huyo hakufaa kupokezwa nafasi hiyo.

Bw Wamumbi sasa atapambana na wawaniaji wengine akiwemo Phylis Wambura Maranga maarufu kama ‘Shosh’ ambaye aliwania kiti hicho 2017 na kushindwa pembamba na Bw Gachagua.

Bi Maranga, 74, amepokezwa tikiti ya Jubilee kuwania kiti hicho cha ubunge na atakuwa mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuwania wadhifa wa kisiasa nchini tangu nchi ijinyakulie uhuru.

Wengine wanaolenga wadhifa huo ni Stanley Waruru wa Narc-Kenya cha Martha Karua, Karweru Kiragu wa Usawa Party kinachoongozwa na Gavana wa Murang’a na mwaniaji wa Urais Mwangi Wa Iria.

Aliyekuwa kijana wa mtaani maarufu kama ‘Chokora’ Daniel Kiige pia yupo kiny’ang’anyironi akilenga kuwania kupitia Justice and Freedom Party.

  • Tags

You can share this post!

Pingamizi dhidi ya Sonko hazina msingi – Mbogo

TUSIJE TUKASAHAU: Wakenya walioko katika kambi za IDPs wadi...

T L