Habari Mseto

Wakazi waomba malandilodi wakome kuwaitisha kodi kwani 'hali ni mbaya'

April 20th, 2020 1 min read

NA RICHARD MAOSI

Wakazi katika mtaa wa Langalanga kaunti ya Nakuru wameelezea hofu ya kufurushwa kwenye nyumba za kupangaendapo hawatalipa kodi, wakiwaomba malandilodi waelewe hali ya uchumi ni ngumu na wakome kuwaitisha kodi.

Baadhi ya malandilodi walikuwa wameanza kutoa vitisho kuwa wangeng’oa milango au mabati na kwa sasa wakazi,wanataka serikali ya kaunti kuingilia.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali wapangaji wanasema, tayari wenye nyumba walikuwa wameanza kuitisha kodi za nyumba na kuweka makataa ya saa chache kabla ya kuwatimua.

Mmoja wao anasema amekua akiishi Langalanga tangu 1998, lakini alisimamishwa kazi wiki mbili zilizopita.

“Nilikua nikifanya kazi katika saluni mjini Nakuru, lakini tangu gavana Lee Kinyanjui apige marufuku shughuli za ususi, ilibidi mwajiri wangu anisimamishe kwa muda,” akasema mkazi huyo ambaye aliomba jina lake libanwe.

Aliongezea kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa hivi, basi Wakenya wajiandae kwa hali ngumu ya maisha siku za baadae

Anaomba serikali iingilie kati ili kukomboa raia mwenye kipato kidogo waweze kupata chakula, maji na mahitaji mengine ya kimsingi .

Aidha alisema wakati huu mgumu wamiliki wa nyumba wanastahili kuelewa kuwa hali ya uchumi ni ngumu kwa kila raia wakati huu ambapo taifa linapigana na janga la Covid -19.

Aidha aliongezea kuwa alikuwa na watoto watatu  pamoja na mke waliokuwa wakimtegemea kwa kila kitu.

Hili linajiri siku chache baada ya katibu mkuu wa miungano ya wafanyikazi (COTU) Francis Atwoli kuwarai wamiliki wa nyumba kutoitisha kodi kutoka kwa wapangaji kwa miezi mitatu ili kuwapuguzia mzigo wa gharama ya Maisha wakati huu ambapo uchumi unaendelea kudorora.

Atwoli alisema angesaidia kushirikisha serikali kuu ili kuwaokoa wafanyikazi wengi ambao walikuwa wamepatiwa likizo ya lazima bila malipo tangu janga la Corona kutokea.