Habari

Wakazi waombwa kuhifadhi maji na chakula kwa matayarisho ya msimu wa kiangazi

January 9th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

MAAFISA wa asasi muhimu wanawataka wakazi wa maeneo ya Pwani na kote nchini kuhifadhi chakula cha kutosha kuepuka baa la njaa msimu wa kiangazi unapoingia.

Katika taarifa iliyochapishwa na idara ya hali ya hewa nchini, raia wameshauriwa kujitayarisha na msimu huo ambao utadumu kwa muda wa miezi mitatu.

Watabiri hao wanasema hali hiyo itashuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi.

Naibu mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa Bw Benard Chanzu alisema kuwa nchi haitashuhudia ukame lakini kutakuwa na uhaba wa chakula kufutia jua kali linalotazamiwa katika sehemu nyingi za nchi.

“Msimu wa kiangazi unatazamiwa kudumu kwa muda wa miazi mitatu, ndani ya muda huu baadhi ya vyakula na mboga vinavyotegemea mvua kunawiri vitapotea,” akaeleza Bw Chanzu.

Mkurugenzi wa shirika hilo katika Kaunti ya Mombasa Bw Charlse Mwangi, alisema japo msimu huo hautaleta ukame, wakazi watashuhudia upungufu wa baadhi ya vyakula.

“Tumetoka katika msimu wa mvua. Watu wengi wanadhani msimu huu utadumu kwa muda mrefu. Wakazi wanapaswa kujitayarisha kwa kuhifadhi chakula ili kuepuka makali ya njaa,” akasema.

Alisema msimu huo utadumu kutoka mwezi wa Januari hadi mwishoni mwa mwezi Machi.

Aidha amewaonya wakazi dhidi ya kutembea wakati wa jua kali akisema kufanya hivyo ni kudhuru afya zao.

“Tunapaswa kulinda ngozi zetu dhidi ya miale ya jua ambapo sasa hivi ni mikali mno na inaweza kusababisha maradhi ya ngozi, kiharusi joto, ugonjwa wa macho kufuatia vumbi jingi na maradhi mengineyo yanayotokana na joto kali,”akaeleza.

Pia aliwaomba wafugaji kuweka chakula cha wanyama wao ili kuepuka migogoro na majirani zao kuhusu chakula cha wanyama hao.

“Tumekuwa tukishuhudia uhasama baina ya wakulima na wafugaji. Hali hii itaweza kuepukika iwapo wafugaji watahifadhi chakula cha kutosha wakati huu ambapo nyasi zimejaa,” akasema Bw Mwangi.

Mkurugenzi huyo pia aliwapa tahadhari wakazi wa Mombasa akisema watarajie kuongezeka kwa bei za chakula hasa mboga.

“Kiangazi kitakapoingia baadhi ya vyakula vitakauka hivyo bei ya chakula itaongezeka,” akasema.

Aliwashauri wakazi kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye mito itakapokauka.

Aliwaomba watakaozuru fuo za Bahari Hindi kuzingatia kwenda sehemu hizo wakati wa jioni ambapo jua huwa limepungua makali.

Mombasa na Pwani kwa jumla imekuwa ikishuhudia mafuriko baada ya mvua iliyonyesha kuanzia Oktoba 2019.

Hali hiyo ilisababisha barabara nyingi ziziweze kupitika kufuatia maji mengi yanayokaa katika barabara hizo.

Sehemu zilizoathirika zaidi ni Nyali, Kisauni, Kongowea, Kaa Chonjo na sehemu zinginezo.