Habari

Wakazi waponea ukuta wa jumba ukiporomoka

May 8th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAKAZI wa jumba moja katika mtaa wa Ruaka, Kaunti ya Kiambu, Jumatano asubuhi walinusurika maporomoko ya ardhi yaliposababisha sehemu ya kuegesha magari kudidimia.

Ukuta uliokuwa umelizunguka jumba hilo uliporomoka, pamoja na sehemu ya maegesho ya magari kutokana na kinachoaminika kuwa ukiukaji wa sheria za ujenzi na mwanakandarasi wa jengo lililo mkabala na jumba hilo.

Jana, uchunguzi ulikuwa ukifanywa kubainisha ikiwa ni salama kwa wakazi kuendelea kuishi hapo.

Wakazi wa jumba hilo linalofahamika kama Grafions, Lane 26, Ruaka, waliamshwa na mshindo mkubwa mwendo wa saa nane na robo asubuhi, ambao hawakuweza kujua mara moja ulikotokea.

“Niliamka, nikachungulia nje lakini kwangu mimi, kila kitu kilionekana shwari. Nilirudi kulala lakini nikaamshwa mara moja na mlinzi,” alisema mwenyekiti wa chama cha wakazi wa jumba hilo, ambaye hakutaka jina lake kuchapishwa.

Ni wakati huo ambapo mlinzi alimshauri kwenda kuondoa magari yaliyokuwa kwenye maegesho. Ndani ya maegesho, yalikuwa magari matatu ambayo yalikuwa yakining’inia, moja tayari lilikuwa limeanguka ndani ya shimo karibu na jumba hilo, na lilikuwa limefunikwa kwa mchanga na vifusi.

“Tulifanikiwa kuondoa magari mawili, moja likitushinda, na lingine lilianguka ndani ya shimo,” alieleza. Hata hivyo, gari hilo liliondolewa saa kadhaa baadaye.

Ingawa Mamlaka ya Ujenzi (NCA) iliagiza wakazi kuhama, Taifa Leo ilipozuru ilipata baadhi wakiwa wapo ndani ya nyumba zao.

“Jinsi jumba linavyokaa kwa kuliangalia, limo dhabiti, lakini uchimbaji kando yake, ambao haukufanywa vyema umeliathiri,” alisema Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kukagua Majumba (NBI), Bw Moses Nyakiongora.