Habari za Kitaifa

Wakazi wasema ‘propela ya helikopta ilikwama’

April 19th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

WAKAZI zaidi ya 20 walio wanachama wa ardhi ya jamii ya Sindar ambapo ajali iliyomuua Jenerali Francis Ogolla ilitokea Alhamisi walisema propela ya helikopta aliyosafiria akiwa na wenzake ilitoa sauti isiyo ya kawaida kabla ya kuanguka.

Wanachama hao walikuwa wakiandaa ardhi ya jamii hiyo kwa upanzi wakati ajali hiyo ilipotokea.

“Ilikuwa mwendo wa saa nane na dakika 50 mchana tulipoona helikopta ikianguka kwa sauti ya kishindo, tulikimbia hadi eneo la tukio na kuanza kuwaokoa waliokuwa ndani wasiungue kwa moto mkali uliokuwa ukiwaka ilipoanguka,” alisema Cregory Boen mwanachama wa jamii ya Sindar.

Bw Boen ambaye alisimulia jinsi walivyotumia panga kukata mikanda ili kuondoa miili kutoka kwa ndege alisema kabla ya ajali hiyo propela ya ndege ilikuwa ikitoa sauti ya ajabu.

“Ingawa mimi si mtaalamu wa masuala ya ndege lakini kwa uelewa wangu ilikuwa ikitoa sauti ya ajabu na propeli ilifeli na ndege ikaanguka,” alisema Boen.

Bw Boen alikumbuka kwamba mmoja wa manusura ambaye alikuwa amevunjika mguu alilia akiomba msaada.

Alisema walimwokoa kutoka kwa ndege hiyo kabla ya maafisa wa Jeshi kukita kambi eneo hilo na kuwaagiza wananchi kuondoka eneo hilo.

“Mtu tuliyemuokoa alikuwa na kamera kama hii yenyu, nadhania alikuwa mwandishi wa habari kama wewe,” alisema Bw Boen. Kulingana na Bw Boen ndege hiyo ilitoa sauti ya ajabu huku propela ikifeli.

“Sijawahi kuona helikopta angani ambayo propela haisogei. Kulingana na mimi, huenda ilipata hitilafu za kiufundi kabla ya ajali,” aliongeza Bw Boen.

Mtu mwingine aliyeshuhudia tukio hilo alisema helikopta hiyo ilitoa sauti isiyo ya kawaida kabla ya kushuka na mlio kwa kishindo.

Alex Kosgei alisema sauti iliyotolewa na helikopta hiyo ilikuwa ya kushangaza sana na ya kutisha. Bw Kosgei alisema kabla ya ajali hiyo ndege ilikuwa ikitembea polepole sana.

“Ndege ilikuwa ikitembea polepole sana na haikuwa juu sana, sijawahi kuona ndege ikienda jinsi ndege hii ilivyokuwa ikienda,” alisema Bw Kosgei huku akionyesha eneo la ajali.

Wakati huo huo maafisa wa uchunguzi kutoka KDF walifika eneo la ajali mwendo wa saa 10:40 asubuhi siku ya Ijumaa kuanza kukusanya taarifa kutoka eneo la tukio na pia kuokota mabaki ya ndege kwa uchunguzi wa kitaalamu.

Wananchi na waandishi wa habari walizuiwa kufika eneo la tukio. Kikosi cha maafisa wa Jeshi wamekuwa wakipiga kambi katika eneo la tukio tangu ajali hiyo itokee.