Makala

Wakazi wasifia Achani kwa kutumia usafiri wa umma: “Anajali rasilmali za kaunti”

May 27th, 2024 2 min read

NA SIAGO CECE

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale hivi karibuni imevutia hisia mbalimbali kutoka kwa umma, kwa njia ya kipekee ya usafiri inayotumiwa na Gavana Fatuma Achani na baraza lake la mawaziri.

Bi Achani ambaye kwa kawaida angetumia gari lake rasmi na nyingine kwenye msafara kukagua miradi, aliamua kutumia basi la serikali ya kaunti kwa pamoja na baraza lake la mawaziri na maafisa wengine wa kaunti.

Kulingana na serikali ya kaunti, hatua hii ni sehemu ya hatua za kaunti kupunguza matumizi ya fedha.

Kiongozi huyo wa kaunti pia amekuwa akipunguza matumizi ya fedha kwa kukwepa kuandaa mikutano katika hoteli za kifahari zilizo Diani.

Katika hafla ya hivi majuzi akielekea katika chemchemi za Maji Moto katika Kaunti Ndogo ya Lungalunga, alipanda basi moja na Naibu wake Chirema Kombo na mawaziri wa kaunti, ambao pia kwa kawaida wangesafiri kwa magari mengi, pamoja na wafanyikazi wengine wa kaunti.

Kisha Bi Achani aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri katika ukumbi kwenye mradi unaoendelezwa eneo hilo.

“Hii ni sehemu ya juhudi za utawala kupunguza matumizi ya fedha za serikali na kuelekeza fedha kwa maendeleo,” alisema msemaji wa Kaunti ya Kwale Nicky Gitonga.

Ndani ya basi, Bi Achani aliketi katikati na walinzi wake wawili wakiwa wamekaa nyuma yake. Wajumbe wengine walikalia viti vingine kwenye basi hilo.

Gavana wa Kwale Fatuma Achani, walinzi wake na maafisa wengine wa kaunti wakisafiri katika basi kuelekea mkutano wa baraza la mawaziri wa Kaunti ya Kwale. Picha|Cece Siago

Hata hivyo, duru za ndani ya kaunti hiyo zilisema kuwa uongozi huo unakabiliwa na tatizo la pesa na hivyo kutatiza utendakazi katika baadhi ya idara.

Taifa Leo pia imebaini kuwa, mishahara ya baadhi ya wafanyakazi wa kaunti ilikuwa imecheleweshwa kwa wiki kadha.

Baadhi ya wakazi na mashirika ya kijamii walipongeza hatua ya gavana huyo wakisema haionyeshi tu unyenyekevu wake bali pia haja yake ya kujua jinsi rasilimali za umma zinavyogawanywa katika kaunti.

“Hii ni ishara ya unyenyekevu kutoka kwa mkuu wa kaunti, kama kiongozi ni vyema akajidhihirisha kuwa yuko katika ngazi sawa na wakazi anaowatumikia, hii pia inadhihirisha kuwa viongozi wengine katika serikali yake hawapaswi kufanya ubadhirifu,” alisema Rehema Mwachirea, mkazi.

Kwa upande wake, Abdulmalik Fumbwe alisema gavana huyo akichagua kutotumia gari lake rasmi ina maana anataka kupata uzoefu wa barabara na rasilimali nyingine za kaunti.

“Basi ambalo gavana alitumia hukopeshwa kwa wakazi wengine wakati wa shughuli. Hii inaonyesha kuwa sasa anajua hali yake na ikiwa inafanya kazi vizuri na ikiwa inahitaji marekebisho,” alisema Bw Fumbwe.

Aliongeza kuwa, Bi Achani kwa kutumia basi hilo barabarani kutamsaidia kujua hali ya barabara hizo na kuzifanyia ukarabati ipasavyo.

“Hii imeleta matumaini makubwa kwetu kwa sababu inaonyesha kwamba hana ubadhirifu na ni rahisi kwake kushuka hadi katika kiwango chetu,” aliongeza Bw Fumbwe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Bongwe Gombato.

Mwenyekiti wa Kamati ya Makubaliano ya Maendeleo ya Jamii (CDAC) ya Msambweni, Jamal Kidyogo alisema hatua ya hivi majuzi ya Bi Achani imeonyesha nia ya kutumia vyema rasilimali katika kaunti yake.

“Hii inaonyesha kwamba anajali rasilimali za kaunti. Ukweli kwamba alitumia basi moja na wafanyakazi wake pia inaonyesha kuwa yeye ni mtu wa kufikiwa kwa urahisi,” alisema Bw Kidyogo.

Aliongeza kuwa uwepo wake kwenye eneo hilo utasaidia chemchemi za maji moto kufahamika kama kivutio kikuu cha watalii.