Habari Mseto

Wakazi wataka kesi yao iende kwa Maraga

November 6th, 2020 2 min read

Na PHILIP MUYANGA

BAADHI ya wakazi katika mtaa wa Buxton, Kaunti ya Mombasa ambao wanapinga mradi wa nyumba za kisasa wa Sh6 bilioni, wanataka kesi hiyo iwasilishwe kwa Jaji Mkuu na kusikilizwa na majaji wasiopungua watatu.

Mradi huo unaendeshwa na serikali ya kaunti ikishirikiana na mwekezaji wa kibinafsi.

Wakazi hao ambao ni wapangaji katika mtaa huo wanasema kuwa ombi lao linaibua swali muhimu, kuhusu iwapo serikali ya kaunti ina uwezo kisheria wa kumkabidhi mtu binafsi ardhi ya umma.

Kupitia kwa wakili Gikandi Ngibuini, wakazi hao wanasema kesi hiyo si rahisi kwa kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa na kampuni ya Buxton Point Apartment Ltd wameshirikiana.

“Ni wazi kwamba hakuna uamuzi wowote ulitolewa na korti yeyote kuhusu suala kama hilo, kwa hivyo inafaa kesi hiyo iwasilishwe mbele ya majaji watakaochaguliwa na Jaji Mkuu,” akasema Bw Ngibuini katika ombi hilo.

Bw Ngibuini alisema pia kuwa ombi hilo linakusudia kutetea haki za kimsingi na pia linashughulikia suala la maadili ya kitaifa na kanuni za utawala.

Alisema kuwa ombi hilo pia linaathiri maisha ya zaidi ya wakazi 500 ambao wanaishi katika eneo hilo la Buxton, na matokeo yake yatakuwa na athari kubwa kwa wapangaji wengine wengi ambao wanaishi katika nyumba za manispaa kote nchini.

“Kwa hivyo, ni sawa na haki kwamba ombi hili liamuliwe na angalau majaji watatu,” akasema.

Hata hivyo, serikali hiyo ya kaunti inasema ombi la wakazi hao halionyeshi suala lolote kubwa la kisheria, linaloweza kuifanya kesi hiyo kuwasilishwa kwa Jaji Mkuu.

“Ombi lao halizungumzii suala lolote ambalo linaibua mambo makubwa kisheria yanayofaa kusikilizwa na kuamuliwa na jaji zaidi ya mmoja wa korti hii,” ikasema serikali ya kaunti hiyo.

Kwa upande wake, kampuni ya Buxton Point Apartment Ltd inasema nguvu zinazotumiwa na jaji mmoja au zaidi wenye mamlaka ya kiwango kimoja ni sawa, kwani hakuna aliye bora kuliko mwingine.

Kampuni hiyo ilisema kwamba hakuna umuhimu wa kuiuliza korti iamue ikiwa umiliki wa ardhi ambayo inamilikiwa na mtu binafsi au shirika, kama ni ardhi ya umma au ya kibinafsi.

Katika ombi lao, wakazi wanataka korti iseme kuwa wana haki ya kuendelea kuishi katika nyumba hizo, na kwamba serikali ya kaunti na kampuni ya Buxton Point Apartment Ltd ambayo inafaa kutekeleza mradi huo, hawana nguvu ya kuingilia utulivu na amani walionayo wakiishi pale.

Wapangaji hao wanahofia kuwa hawataregeshwa tena katika nyumba zao, ambazo zinatarajiwa kubomolewa na zile zitakazojengwa zitauzwa kwa watu wengine wenye pesa.