Habari

Wakazi wataka mgao katika bandari Lamu

October 4th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SHINIKIZO zinazidi kutolewa kwa serikali kuitengea kaunti na jamii ya Lamu asilimia 25 ya mapato katika mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (Lapsset), itakapoanza shughuli zake rasmi.

Kiegesho cha kwanza cha bandari hiyo kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mwezi huu wa Oktoba kuashiria mwanzo wa shughuli za bandari hiyo.

Kupitia wanachama wa Jukwaa la Lamu, ambayo ni bodi inayojumuisha Baraza la Wazee wa Lamu, Sauti ya Wanawake wa Lamu, Vijana na pia wanaharakati wa kijamii, walisema ipo haja ya serikali kuu kuitengea Kaunti ya Lamu asilimia 25 ya mapato.

Asilimia 20 walisema itaelekezwa moja kwa moja kwa serikali ya kaunti kutekelezea miradi ya maendeleo.

Asilimia tano iliyosalia walipendekeza ielekezwe kwa jamii ya Lamu kupitia wakfu maalum wa maendeleo ya jamii eneo hilo; ya Lamu Community Trust Fund.

Msemaji wa Jukwaa la Lamu, Bw Mohamed Abubakar, ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa kutetea haki za kijamii wa Save Lamu, alimuomba Rasi Uhuru Kenyatta kuhakikisha anakutana na jamii ya Lamu kwanza ili kuarifiwa malalamishi kuhusu LAPSSET kabla ufunguzi wa kiegesho cha kwanza.

Bw Abubakar alisema mbali na Lamu kutengewa asilimia 25 ya mapato ya kodi kutoka LAPSSET, jamii pia inashinikiza wavuvi zaidi ya 4,000 walioathiriwa kufidiwa kikamilifu kwanza kabla ya shughuli za mradi huo kuanza.

“Tunamuomba Rais Uhuru Kenyata kusikia kilio cha watu wa Lamu. Ombi letu ni jamii ya Lamu ifaidike moja kwa moja na mradi wa Lapsset ambao uko eneo letu,” alisema.

Aliongeza: “Tunataka kuona angalau asilimia 25 ya mapato ya kodi kutoka Lapsset inabaki hapa Lamu ili kuendeleza miradi ya kaunti na kufaidi jamii husika. Msimamo wetu ni kwamba kabla ya kiegesho cha kwanza kilichokamilika kuzinduliwa, wavuvi wetu zaidi ya 4,000 wafidiwe kwanza.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Lamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Sharif Salim, alisema msimamo wao pia ni kamati maalum itakayotetea haki za jamii ya Lamu kwenye mradi wa Lapsset ibuniwe kwanza kabla ufunguzi wa shughuli za bandari kutekelezwa.

“Tunataka kamati maalum ibuniwe ili kutetea haki za jamii yetu wakati mradi wa Lapsset utakapokuwa ukiendeleza shughuli zake hapa,” akasema Bw Salim.

Naye Bw Mohamed Athman, pia alishikilia kuwa lazima nafasi 1,000 za vijana wanaostahili kufadhiliwa na serikali kupitia wakfu wa Rais na mradi huo wa bandari, itekelezwe kikamilifu kabla ya shughuli za bandari kuzinduliwa.

Wanachama wa baraza hilo pia wanashinikiza kuwe na mpango maalum wa kuhakikisha vijana wa Lamu waliohitimu wanapewa nafasi za kwanza za ajira kwenye mradi wa Lapsset.

Mradi huo wa Lapsset ambao pia unajumuisha ujenzi wa barabara kadha zinazounganisha Kenya na Sudan Kusini na pia Ethiopia, mabomba ya mafuta, miji mikuu, viwanja vya ndege na reli, umeibua matumaini makubwa miongoni mwa wakazi wa Lamu, hasa katika kuinua uchumi wake.