Habari Mseto

Wakazi wataka upatikanaji suluhu kwa masaibu yatokanayo na bwawa la Masinga

March 4th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ekalakala, Masinga, Kaunti ya Machakos, wanalalamika kutokana na watu kuangamia katika bwawa la Masinga.

Wakazi hao wamesema kwa miezi michache iliyopita wakazi kadhaa na wanafunzi wameshambuliwa na kiboko na mamba ambao ni wengi katika bwawa hilo.

Wameikosoa kampuni ya umeme ya KenGen kwa kukosa kuwapa fidia ya masaibu hayo wanayopitia.

Wamesema hivi majuzi kijana mwenye umri wa miaka sita wa Shule ya Msingi ya Isyukoni alishambuliwa na mamba na kupatikana baada ya wiki moja.

Mkazi mwingine alishambuliwa na kiboko kutoka kijiji cha Ekalakala alipokuwa amekwenda kutega samaki, huku watoto wa shule wengi wakisombwa na maji wanapovuka bwawa hilo wakienda shuleni.

Wakazi hao wanalalamika ya kwamba kwa muda mrefu hawajapata kivukio cha kuwapeleka kaunti jirani ya Embu na hata Murang’a.

Hata hivyo, naibu kamishna wa Masinga Bw John Ayenda, amewashauri wakazi hao kuwachunga wana wao wakati wowote wanapokwenda shuleni.

“Kila mzazi ni sharti awe makini na mwanawe kila mara wanapokwenda ng’ambo ya pili ya bwawa hilo,” akasema Bw Ayenda.

Tayari wakazi hao waliwachagua wawakilishi wawili ambao watapeleka matakwa na malalamiko yao kwa kampuni hiyo ya KenGen.

Bw Peter Kitonyi na Bi Ruth Munini Nzomo walichaguliwa na wakazi hao ili wawe kama wawakilishi wao kwa kampuni hiyo.

Baada ya mkutano ulioandaliwa wawili hao walipewa jukumu wawe macho ya wakazi hao ambapo wakati wowote kukiwa na mkutano wa bodi ya kampuni hiyo, watakuwa mstari wa mbele kuwasilisha matakwa ya wananchi.

Wakazi hao walisema wanapitia masaibu mengi ambapo licha ya kampuni hiyo kuwa katika vipande vyao vya ardhi bado wakazi wengi hawajapata umeme katika nyumba zao.

Wakazi hao walisema vijiji vilivyoathirika sana na masaibu hayo ni Ekalakala na Wamboo huku wakisema watu wengi wamesombwa na maji na hata kushambuliwa na mamba hasa majira ya jioni.

Walisema hata wakazi wengi ambao huenda kunyunyizia mashamba yao maji karibu na bwawa hilo wameangamizwa na viboko ambao hujificha kanda ya bwawa hilo mchana.

Bw Francis Kilango ambaye ni mkazi wa Ekalakala anaiomba serikali kupitia kampuni hiyo kufanya hima ili kuokoa wakazi hao kutokana na masaibu hayo.

“Sisi kama wakazi wa eneo hili tumepitia shida nyingi sana ambapo inabidi watu kukaa karibu na bwawa hilo kwa vikundi ili kupambana na wanyama hao wakati wowote ule. Hatungetaka watu wetu wazidi kupotelea kwenye bwawa hili. Ni vyema hatua ya haraka ichukuliwe,” akasema Bw Kilango.