Wakazi watakiwa kusubiri picha rasmi ya Ruto

Wakazi watakiwa kusubiri picha rasmi ya Ruto

NA KENYA NEWS AGENCY

NAIBU Kamishna wa Nyahururu, Bw Ndambuki Muthike, ameomba wakazi na maafisa wa serikali kusubiri picha rasmi za rais za kuweka katika biashara na ofisi zao.

Afisa huyo alisema hayo huku wafanyabiashara wakichapisha kadhaa na kuuzia wakazi wanaozihitaji kwa wingi.

Akiwataka wakazi, machifu na maafisa wengine wa serikali kutonunua picha hizo kutoka barabarani, Bw Muthike alisema zitachapishwa na mchapishaji wa serikali na kusambaziwa ofisi zote za umma kupitia idara ya habari.

“Hata mimi nimeondoa picha ya Rais mstaafu Uhuru na ninasubiri ya rais mpya,” alisema Bw Muthike, na kuhimiza idara ya habari kuharakisha mchakato wa kusambaza picha hizo.

Muthike pia alikiri kwamba aliuziwa picha isiyo rasmi lakini akakataa kununua.

Picha hizo zinauzwa katika maduka kadhaa mjini Nyahururu kwa kati ya Sh400 na Sh1,500 kwa kutegemea saizi yake.

“Wakazi wamekuwa wakifika hapa kwa wingi kutafuta picha rasmi na tumelazimika kuchapisha kitu waweze kununua. Tunafahamu kwamba hizi sio picha rasmi lakini lazima tukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wateja,” alisema mfanyakazi katika Annex Photo Studio mjini humo.

  • Tags

You can share this post!

Kesi ya ‘mwana’ wa Kibaki yatupwa

TAHARIRI: Kaunti zina jukumu kubwa kuzima njaa

T L