Habari Mseto

Wakazi waonywa dhidi ya kutumia majanichai kutibu macho mekundu

January 25th, 2024 2 min read

BAADHI ya wakazi wa Mombasa wameamua kujitibu nyumbani ugonjwa wa macho mekundu ambao unazidi kuenea maeneo ya Pwani.

Mbinu ambazo zimegunduliwa kutumiwa ni pamoja na uoshaji macho kwa kutumia mchanganyiko wa majanichai, au maji ya chumvi, na wengine wanatumia mitishamba.

Wataalamu wa matibabu wa macho wametaja mbinu hizi kuwa hatari, zinazoweza kusababisha madhara ya kudumu.

Wakazi waliohojiwa na Taifa Leo walisema waliamua kuchukua mwelekeo huo baada ya dawa za dukani kukosa kuwatibu.

Bi Flora Naomi, msanii wa vipodozi anayeishi Bamburi katika siku nne zilizopita amekuwa akitumia ‘chai kali’ kunawa uso na macho kama matibabu ya ugonjwa wa macho.

“Imekuwa tukio lisilofurahisha sana lakini nimekuwa nikichemsha majani ya chai yaliyokolezwa na kuyaacha yapoe kabla ya kuosha macho asubuhi na jioni hadi sasa niko sawa,” Bi Naomi alisema.

Anashuku kuwa alipata maambukizi hayo alipokuwa kazini katika Kaunti ya Kilifi.

“Nilifikiri nilikuwa nageuka kipofu. Mwasho ulikuwa mbaya sana na nilitumia dawa lakini sikupata matokeo yaliyotarajiwa,” aliongeza.

Bi Serah Waithira Kahiu, mwanasayansi, alisema baadhi ya watu wanapendelea kuweka mfuko wa chai kwenye kope kwa muda wa dakika tano na wengine humimina matone ya chai ndani ya macho.

Soma Pia: Namna ya kuepuka ugonjwa wa macho mekundu

Tiba nyingine ambazo wakazi wameamua kuzitumia ni pamoja na kutumia maji ya chumvi hutengenezwa nyumbani au hutolewa kutoka baharini.

Kulingana na Dkt Ibrahim Matende, mbinu hizo zinaweza kupunguza maumivu lakini zikaachia mtu madhara ya kudumu ikiwemo uwezekano wa kuwa kipofu.

Dkt Matende alisema maradhi ya macho ambayo yanashuhudiwa sasa, hupona yenyewe hata bila kuhitaji dawa.

Alisisitiza kuwa, jambo la muhimu ni kwa wakazi kufuata ushauri wa kudumisha usafi hasa wa mikono na kutogusagusa au kusugua macho yao.

“Ikiwa ni lazima uweke chochote, tumia maji safi kuosha macho yako. Watu wengine hata hutumia mkojo au maziwa ya mama… hii ni suluhu ya muda mfupi ya kutuliza maumivu tu. Konea, ikiwa itaathiriwa na ikiwa haitatibiwa kwa wakati, unaweza kuwa kipofu,” alisema Dkt Matende.

Hata hivyo, wakazi wanaendelea na maisha yao ya kawaida huku majengo machache tu yakiweka ilani na sabuni za kunawa mikono milangoni.