Wakazi waulizia aliko gavana wao

Wakazi waulizia aliko gavana wao

NA GEORGE ODIWUOR

WAKAZI wa Kaunti ya Homa Bay wamezua maswali kutokana na kutoonekana hadharani kwa Gavana Cyprian Awiti wakati ambapo huduma mbalimbali zinaendelea kudodora huku migomo ya wahudumu wa afya bado ikiendelea.

Mara ya mwisho Bw Awiti kuonekana hadharani ni wakati wa mazishi ya aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Saudi Arabia marehemu Paddy Ahenda. Mazishi hayo yalihudhuriwa na Kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ambaye ni mshirika wa karibu wa gavana huyo.

Kabla ya kuhudhuria mazishi hayo, Bw Awiti hakuwa ameonekana hadharani kwa wiki kadhaa na kuzua maswali kuhusu yanayoendelea kwenye kaunti hiyo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Bunge la Wenye Nchi Homa Bay Walter Opito na Mshirikishi wa masuala ya kijamii Evans Oloo anayesimamia kaunti hiyo sasa haijulikani kwa sababu hata wahudumu wa afya wanaoshiriki migomo hawana wa kuwasikiza na kutilia manani masaibu yao.

Wawili hao walisema kuwa kutoonekana kwa Bw Awiti pia kumesababisha baadhi ya wafanyakazi wa kaunti hiyo kukosa kufika kazini kwa sababu hakuna anayefuatilia utendakazi wao.

“Naibu Gavana Hamilton Orata pia hajakuwa akifika katika afisi yake. Nina hakika kuwa kuna mawaziri wengi wa kaunti na wakuu wa idara mbalimbali ambao pia huwa hawafiki kazini,” akasema Bw Oloo.

Kulingana na wapiganiaji hao wa haki za kibinadamu, hata wafanyakazi wa vyeo vya chini wameanza kufika kazini wakiwa wamechelewa nao wengine hawaendi kabisa kutoa huduma zao.

“Huenda ikafika wakati ambapo afisi nazo zitafungwa kwa sababu wafanyakazi nao wanafuatilia iwapo gavana anafika kazini au la. Huduma nazo zinaendelea kudorora kutokana na gavana kutoonyesha uongozi bora,” akaongeza Bw Oloo.

Katika muhula wake wa kwanza kati ya 2013-2017, Bw Awiti alizindua miradi mbalimbali ya kustawisha kaunti hiyo kiuchumi na pia ujenzi wa viwanda.

Kati ya miradi hiyo uzinduzi ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza vyakula vya mifugo eneo la Arujo viungani mwa mji wa Homa Bay na kile cha kusaga mahindi kinachopatikana Kigoto, Suba. Hata hivyo, miradi hiyo imekwama wala haijamalizwa kwa wakati.

Viwanda vingine kama kile cha kutayarisha viazi vitamu kilichostahili kujengwa katika eneobunge la Kasipul Kabondo na mananasi katika eneobunge la Rangwe hadi leo ujenzi wao haujaanza.

“Kile ambacho hangeweza kufanya kwa muda wa miaka tisa iliyopita hawezi kukamilisha kwa muda wa miezi mitatu,” akasema Bw Oloo huku akionekana kukata tamaa na uongozi wa Bw Awiti.

Mkazi Tom Mboya naye anasema kuwa Bw Awiti hajali iwapo watu wanapokea huduma katika serikali yake au la kwa sababu anastaafu na hatafuti tena cheo chochote.

Hata hivyo, afisa mmoja wa kaunti ambaye hakutaka anukuliwe alisema Bw Awiti amekuwa akitekeleza majukumu yake na akawapuuza wanaosema amewatelekeza wakazi. Alisema mekuwa akishiriki shughuli mbalimbali ikiwemo mkutano wa Baraza la Magavana hivyo kutofika afisini hakumaanishi kuwa hafanyi kazi.

You can share this post!

Karua atoa ahadi ya kuzidi kutetea wanawake wote

Wawaniaji 16 wa urais wawasilisha saini zao kwa IEBC

T L