Wakazi wavamia kasisi anayedaiwa kulawiti wavulana

Wakazi wavamia kasisi anayedaiwa kulawiti wavulana

Na GERALD BWISA

WAKAZI wenye ghadhabu Jumamosi walivamia kanisa la Rise Up Society Mission linalomilikiwa na kasisi anayedaiwa kuwa na mazoea ya kulawiti wavulana mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Wakazi waliwashutumu maafisa wa usalama kwa kushindwa kumkamata kasisi Jimmy Nduruchi hata baada ya kupiga ripoti mara kwa mara kwa polisi.

“Kasisi huyo anaendelea kulawiti wavulana hata baada ya waathiriwa kuripoti kwa Kituo cha Polisi cha Kitale,” akasema Bw Silus Wafula, mwanaharakati.

Wakazi jana walisema kuwa polisi hawajachukua hatua licha ya kukabidhiwa ushahidi wa mazungumzo ya simu na video.

“Watu wengi, wakiwemo viongozi wa eneo hili, wamekuwa wakilalamikia dhuluma zinazotekelezwa na kasisi huyo dhidi ya watoto lakini polisi hawajamchukulia hatua zozote,” akasema Bw Wafula.

Wakazi wanadai kuwa kasisi huyo amekuwa akiwafanyia wavulana hao unyama huo kwa kujifanya kwamba anawapa msaada.

“Kasisi huyu ana mtandao ambao unasajili watoto wetu ambao mwishowe anawalawiti, lakini maafisa wa polisi wamenyamaza kimya,” akasema Bi Ann Natondo, ambaye ni mkazi.

Viongozi wa kidini, wakiongozwa na Kasisi Andrew Wafula wa kanisa la United Christian Ministries, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Baraza la Makasisi Kaunti ya Trans Nzoia, alitaka Pasta Nduruchi afurushwe kutoka kaunti hiyo.

“Ametia doa kazi ya Mungu katika Kaunti ya Trans Nzoia na hatutamkubalia kufanya tabia inayokinzana na mafundisho ya Biblia,” akasema Kasisi Wafula.

Hayo yanajiri huku waathiriwa wakidai kwamba wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa Nduruchi na sasa wanataka taasisi ya kulinda mashahidi nchini kuingilia kati ili kuwanusuru.

“Watu wa kasisi huyo walikuja nyumbani kwetu huku wakiwa na kamera na kunilazimisha kurekodi video nikisema kwamba nilitoa taarifa ya kupotosha kwa polisi. Lakini nilikataa na wakanipiga vibaya sana,” akasema mmoja wa waathiriwa.

Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), Kaunti ya Trans Nzoia, Francis Kihara, akiwataka wakazi kutojichukulia sheria mikononi na badala yake watoe fursa kwa polisi kukamilisha uchunguzi.

“Waathiriwa wameandikisha taarifa kwetu na tungali tunafanya uchunguzi. Tunahimiza wakazi kuwa na subira,” Bw Kihara akaambia Taifa Leo.

Pasta Nduruchi, hata hivyo, alikanusha madai hayo huku akidai kwamba anahujumiwa na baadhi ya wakazi ambao wanataka hongo.

“Ikiwa madai hayo ni ya kweli, mbona hawajaripoti kwa polisi? Hiyo ni hujuma ambayo inalenga kuniharibia jina,” Pasta Nduruchi akasema kwa njia ya simu.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa visa 25 vya ulawiti vimeripotiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Supritendi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitale, Dkt Sammy Masibo, alisema kuwa visa 11 vya ulawiti vimeshughulikiwa hospitalini hapo ndani ya mwaka mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Chama cha RBK chabuni mbinu za kunguruma 2022

LEONARD ONYANGO: Wapigakura wajifunze kutoka ahadi feki 2017