Habari Mseto

Wakazi zaidi ya milioni moja kunywa maji safi Kiambu

July 5th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wapatao milioni moja Kaunti ya Kiambu watanufaika na mradi wa maji uliozinduliwa katika msitu wa Kinale.

Mwishoni mwa wiki katibu katika Wizara ya Maji Bw Joseph Irungu alizuru eneo hilo ili kujionea uzinduzi huo wa maji.

Alisema kwa muda mrefu wakazi wa Lari, Ndeiya na hata maeneo ya Limuru wamekuwa na matatizo ya maji lakini serikali imeingilia kati ili kutatua shida hiyo.

“Serikali inataka kuona ya kwamba kila mwananchi anapata maji karibu na makazi yake. Kwa hivyo, itafanya juhudi kuona ya kwamba kila mwananchi anapata maji katika makazi yake,” alisema Bw Irungu.

Alisema maeneo mengine yanayotarajiwa kupata maji kwa wingi ni bwawa la Bathi, Ndeiya, Limuru, na Lari.

Katibu huyo alizuru pia kampuni ya maji ya Limuru ili kuelewa jinsi inavyosambaza maji hadi maeneo mengine.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alipongeza juhudi za serikali za kusambaza maji katika maeneo muhimu katika kaunti hiyo.

“Ni muhimu kwa wakati huu kusambaza maji kwa wingi kwa wananchi; huu ukiwa mkakati mmojawapo wa kukabiliana na janga hili la corona. Tungetaka kuona kila kijiji kikiwa na maji ya matumizi,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema jambo muhimu kwa sasa ni kufanya juhudi kuona ya kwamba kila mwananchi anapata maji kwa wingi.

Alisema maeneo wanayolenga zaidi kuyafikia ni katika masoko na maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu.

Alisema idara ya afya ya umma imekuwa mstari wa mbele kupuliza dawa katika sehemu tofauti.

Gavana huyo aliandamana na maafisa wakuu katika kaunti hiyo ambao pia walielezea mikakati walioweka ili kukabiliana na janga la corona.