Dondoo

Wake wazozania mali mara baada ya mume kuzikwa

March 1st, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

KATHIANI, MACHAKOS

KULISHUHUDIWA sinema ya bure eneo hili wake wenza waliporukiana na kuangushiana makonde wakizozania shamba siku mbili baada ya mume wao kuzikwa.

Duru zinasema mume wa akina mama hao aliugua na kuaga dunia. Siku mbili baada ya mwenye nyumba kuzikwa, mke wake wa kwanza aliyekuwa ametoroka alirejea na kudai sehemu ya shamba aliloacha marehemu.

Hata hivyo, mke wa pili alikataa na kumfurusha.

“Wewe, sasa unataka nini hapa. Mume wangu alikutema kitambo na ukaenda kwa wazazi wako. Sasa umekuja kudai nini hapa. Kama unataka shamba hakuna kitu utakachokipata hapa. Nyumba yangu ione paa mara moja kabla sijachukulia hatua kwa kuninyanyasa,” mke wa pili alimwambia mke mwenza.

Hata hivyo, mwenzake alikataa kuondoka.

“Sasa wewe unaniambia nini? Uliolewa juzi na sasa unataka kumiliki mali yote. Haiwezekani hata kamwe, nina haki ya kupata mgao wangu halali,” mama alisema.

Yasemekana hali ilichacha na wawili hao wakaanza kurushiana maneno.

“Huna haya kuja kudai mali baada ya mume wangu kufa. Alipokuwa mgonjwa nilimtunza na wewe haukuja hata kumjulia hali. Nimejua ulikuwa ukiomba afe ili umiliki mali yake. Hilo halitawekezana kamwe,” mke wa pili alimwambia mwenzake.

Kulingana na mdokezi, wawili hao waliamua kudhihirisha ubabe wao kwa kutwangana lakini majirani waliingilia kati na kwenda kuwatenganisha.

Baadaye walishauriwa kufuata sheria ili kutatua mgogoro wao. Mke wa kwanza alisema alikuwa akidai sehemu ya ardhi kwa sababu alikuwa na watoto aliozaa na marehemu naye wa pili akamlaumu kwa kusubiri hadi mwenye boma akafariki.

Haikujulikana kilichojiri baada ya hali kutulia kidogo na wazee wa familia kuingilia kati.